Sehemu ya wakimbiaji wa Mbio za Serengeti Migration Marathon & Anti-Poaching Run wakianza mashindano hayo kwenye uwanja wa Sokoine mjini Mugumu mapema leo asubuhi.
------------------------------------------------
-----------------------------------------------
Vijana walioanzisha na kuendelea kuandaa mashindano ya Mbio za Serengeti Migration Marathon & Anti-Poaching Run, wamepongezwa kwa kuunga juhudi za Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ya Serengeti, Angelina Marko aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi kama mgeni rasmi katika mashindano hayo ya mwaka huu yaliyoanza mapema leo mjini Mugumu, Serengeti.
“Tunawapongeza sana vijana wetu kwa kum- support Rais wetu Dkt Samia katika kutangaza utalii,” amesema DAS Angelina akilenga Filamu ya Royal Tour iliyoandaliwa na Rais Samia mwaka 2022 kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
DAS Angelina akikabidhi zawadi kwa mmoja wa washindi wa mbio hizo leo.
-----------------------------------------------
Pia DAS Angelina amewapongeza vijana hao kwa kutenga asilimia 20 ya fedha za viingilio vya washiriki wa mashindano hayo kwa ajili ya chakula cha wanafunzi na vifaa vya kufukuza wanyamapori waharibifu wilayani Serengeti.
Kati ya asilimia 20 waliyotenga, asilimia 10 imetumika kununua tochi za mwanga mkali na vipaza sauti ambavyo wamevikabidhi kwa kikundi cha vijana wanaojitolea kupambana na wanyamapori waharibifu wilayani Serengeti.
Asilimia 10 nyingine imetumika kununua kilo 600 za mahindi kwa ajili ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Gwazongo, kwa lengo la kuhamasisha wazazi kuchangia chakula cha watoto wao wawapo shuleni.
Mshindi wa kilomita 21 za mashindano hayo, Edward, akimaliza mbio zake kwenye uwanja wa Sokoine mjini Mugumu leo asubuhi.
------------------------------------------------
Mapema, Mratibu wa Mbio za Serengeti Migration Marathon & Anti-Poaching Run, Mwalimu Samwel Mwita Nyankogoti amesema mashindano hayo yalianzishwa mwaka 2020 kutokana na wazo lililobuniwa na vijana wazawa wa wilayani Serengeti.
Mwalimu Nyankogoti akisoma taarifa fupi ya Mbio za Serengeti Migration Marathon leo.
--------------------------------------------------
“Mbio hizi hufanyika kila mwaka kwa siku mbili mfululizo katika maeneo ya mjini Mugumu na Fort Ikoma, zikiratibiwa na Taasisi ya Michezo ya SETSA.
“Lengo kuu la mbio hizi ni kuhamasisha uhifadhi na ulinzi wa ikolojia ya Serengeti pamoja na kutangaza utalii wa ndani na nje ya nchi yetu, hasa magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti,” amesema Mwalimu Nyankogoti.
Amebainisha kuwa jina la Serengeti Migration Marathon limetokana na tukio kubwa na adhimu duniani la uhamaji wa wanyamapori aina ya nyumbu pamoja na wengine wanaofuataa nao zaidi ya milioni 1.5 kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti kwenda Mbuga ya Maasai Mara nchini Kenya kwa kuvuka Mto Mara na kurudi Serengeti kila mwaka.
Picha zote na Mara Online News
-----------------------------------------------
Mashindano ya leo yamefanyika mjini Mugumu kwa mbio za kilomita 21, 10 na tano, ambapo yameshirikisha mamia ya wakimbiaji, wengi wao wakiwa vijana wa kiume na kike kutoka mikoa na taasisi mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Kesho Agosti 4, 2024 yataendelea katika eneo la Fort Ikoma kwa mbio za kilomita 12 na tano, ambapo pia yatashirikisha wakimbiaji kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Grumeti Reserves, Grumeti Fund, TANAPA, TAWA na Ikona WMA.
No comments:
Post a Comment