NEWS

Thursday, 12 September 2024

Diwani atumia mamilioni ya fedha zake kujenga ofisi ya CCM, darasa shule aliyosoma



Muonekano wa mbele wa ofisi ya CCM Kata ya Nyakonga ambayo Diwani Simion Kiles amegharimia ujenzi wake.

Na Mwandishi Maalumu/ Mara Online News

Kuwa kiongozi wa kuchaguliwa ni jambo moja na kuwa kiongozi wa maendeleo ni jambo jingine. Diwani wa Kata ya Nyakonga katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Simion Kiles ameonesha matokeo chanya na mfano wa kuigwa.

Kiles alimaarufu “K”, ametumia fedha zake kugharimia ujenzi wa ofisi ya kisasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nyakonga ili kukipatia chama hicho tawala heshima katika kata yake.

Ujenzi wa ofisi hiyo ambao umegharimu shilingi zaidi ya milioni 90 tayari umekamilika na Kiles sasa anafanya maandalizi ya kuikabidhi rasmi kwa uongozi wa CCM Kata ya Nyakonga.

Kiles ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, anasema alipochaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Nyakonga alikuta haina ofisi ya CCM, jambo ambalo halikumfurahisha.

“Nilikuta hakuna ofisi ya CCM, nikaamua kutumia fedha zangu kutokana na upendo nilionao kwenye chama changu cha CCM kujenga ofisi na sasa imekamilika, ipo inaonekana,” Kiles aliimbia Mara Online News wilayani Tarime juzi.

Diwani wa Kata ya Nyakonga na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles.

Nyakonga sasa inatajwa kama kata yenye ofisi ya mfano sio tu katika wilaya ya Tarime, bali katika mkoa wa Mara ambako ndiko alikozaliwa Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Katibu wa CCM Kata ya Nyakonga, Pius Chacha Nokwe anamshukuru Diwani Kiles akisema wameondokana na adha ya kuendeshea mikutano na vikao vya chama kwenye mabanda.

“Wana-CCM Nyakonga tumefurahi sana, tunamshukuru sana Mheshimiwa Kiles, tunapata sehemu ya kufanyia vikao na mikutano ya CCM, zamani tulifanyia kwenye mabanda ya kuoneshea mpira na wakati mwingine tulichomwa jua na kunyeshewa mvua.

"Sasa tumepata sehemu salama ya kuhifadhi na kutunza nyaraka na kumbukumbu muhimu za chama na jumuia zake. Jengo hili limeking'arisha Chama Cha Mapinduzi, limekuwa kivutio kwa wapinzani kuhamia CCM hapa Nyakonga,” anasema Nokwe.

Diwani Kiles pia ametumia shilingi zaidi ya milioni 40 kugharimia ujenzi wa chumba cha darasa la kisasa na ofisi ya mwalimu (pichani chini) katika Shule ya Msingi Magoto.

“Hii ndiyo shule niliyosoma na nimefurahi kuwajengea darasa na ofisi ya mwalimu, na mbali na samani zingine nitaweka kompyuta kadhaa katika hilo darasa,” anasema Kiles huku akionekana mwenye furaha na ari ya kuendelea kuleta mageuzi ya maendeleo katika kata hiyo.

Kwa mujibu wa Kiles, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imetumia mamilioni ya mapato yake ya ndani kugharimia ukamilishajji wa jengo la utawala na vyumba vinane vya madarasa yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Shule ya Msingi Magoto.

“Kutokana na kazi kubwa iliyokuwa imefanywa na wananchi kujenga maboma, halmashauri yetu iliwaunga mkono kwa kutumia mapato ya ndani kugharimia uezekaji, na mimi nikahamasika kuwajengea darasa na ofisi ambayo ina mpaka choo,” anasema Mwenyekiti huyo wa Halamashauri ya Wilaya ya Tarime.

Kiles anasema alipochaguliwa kuwa diwani alikuta majengo mengi ya shule hiyo ni ya zamani lakini sasa taswira na mazingira ya shule hiyo vinavutia.

Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Magoto, Simion Birai anasema Diwani Kiles ameweka historia ya maendeleo katika kata ya Nyakonga.

"Uwepo wa ofisi imechangia ufanisi katika ufundishaji maana walimu wanapata sehemu ya kufanyia maandalio ya somo, zamani tulitumia darasa kama ofisi na wakati huo huo wanafunzi wakiendelea na vipindi vya masomo.

“Darasa hili ni kwa ajili ya kompyuta, wanafunzi wataanza kusoma somo la TEHAMA, na pia ujenzi huu umekuwa kichocheo cha kuunganishiwa umeme hapa shuleni,” anasema Mwalimu Birai.

Mwalimu Simion Birai

Diwani Kiles anasema anatarajia pia kugawa samani za ofisi (viti na meza) kwa ofisi ya Katibu ya CCM kata ya Nyakonga na jumuiya zake zote.

Aidha, kiongozi huyo ameshanunua viti zaidi ya 300 atakavyovigawa katika vitongoji vyote 12 vya kata ya Nyakonga, ikiwa ni sehmu ya juhudi zake za kuifanya kata hiyo kuwa bora katika huduma kwa wananchi.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages