NEWS

Tuesday, 29 October 2024

Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Musuguri afariki dunia akiwa na umri wa miaka 104, Rais Samia amlilia



Jenerali David Bugozi Musuguri enzi za uhai
---------------------------------------------------------


Na Mara Online News

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) Mstaafu Jenerali David Bugozi Musuguri ameripotiwa kuaga dunia akiwa na umri wa miaka 104 leo Oktoba 29, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, jijini Mwanza.

Kufuatia msiba huo mkubwa kwa Taifa, Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ametuma pole kwa CDF wa sasa na Watanzania kwa ujumla.

"Ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda, Makamanda, wapiganaji wastaafu, wapiganaji walio katika utumishi, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa kuondokewa na shujaa wetu, mpendwa wetu, mwalimu, mshauri na kiongozi wetu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali (Mstaafu) David Bugozi Musuguri.

"Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha yake ya miaka 104, ambapo miaka 46 kati ya hiyo ameitumikia nchi yetu kwa weledi, umahiri, kujituma, ushujaa, nidhamu na kwa mafanikio ya hali ya juu, akiishi kiapo chake cha kuwa tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya ulinzi wa Taifa letu. Ametuachia mfano bora wa utumishi wa umma utakaoendelea kuwa mwanga ndani na nje ya Majeshi yetu.

"Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina," Rais Samia ameandika kwenye ukurasa wake mtandaoni.

David Bugozi Musuguri alizaliwa Januari 4, 1920 Butiama mkoani Mara. Alijiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwaka 1942. Aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi mwaka 1980; wadhifa ambao aliutumikia hadi mwaka 1988.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages