Jenerali David Bugozi Musuguri enzi za utumishi wake jeshini.
Na Mwandishi Wetu
David Bugozi Musuguri, mmoja wa majenerali shupavu wa Tanzania aliyesifika kwa kutopenda masihara katika ulinzi wa taifa na ambaye alishiriki kikamilifu kumng’oa madarakani dikteta Idi Amin wa Uganda alipoivamia Tanzania miaka 45 iliyopita, amefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 104 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mwanajeshi huyo nguli aliyebahatika kuishi kwa zaidi ya karne moja, alizaliwa Januari 4, 1920 katika kijiji maarufu cha Butiama, mkoani Mara.
Alijiunga na jeshi la kikoloni la utawala wa Waingereza la King’s African Rifles (KAR) mwaka 1942 mpaka alipostaafu rasmi mwaka 1988 akiwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania huru.
Kijiji cha Butiama alichokulia Jenerali Musuguri kimejitawalia umaarufu duniani kwa kuwa ndipo mahali alipozaliwa gwiji wa siasa barani Afrika na duniani, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (1922-1999).
Jenerali Musuguri, ambaye alishiriki katika Vita Vikuu ya Pili ya Dunia (1939-1945), anasifika kwa kuyaongoza majeshi ya Tanzania mwaka 1978-1979 kumtimua madarakani nduli Idi Amin Dada wa Uganda alipovamia eneo la Mtukula mkoani Kagera.
Jenerali Musuguri alikuwa mkufunzi wa askari wakati wa ukoloni wa Mwingereza. Mwaka 1953 alimfundisha pia Idd Amin katika kambi ya mafunzo ya Kahawa Barracks nchini Kenya. Hivyo mwaka 1978 katika vita vya Kagera, Mwalimu [Musuguri] aliingia vitani na mwanafunzi wake [Amin] na akamshinda.
Amin, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Jenerali Musuguri, alisalimu amri na kukimbilia Saudi Arabia ambako aliishi miaka kadhaa na kufariki dunia.
Miaka minne iliyopita wakati Jenerali Musuguri alipohojiwa baada ya kutimiza umri wa miaka 100 alisema hakutarajia kufikia umri huo zaidi ya kupata matunzo mazuri kutoka kwa jamii na taifa.
Mwandishi wa habari wa Gazeti la Serikali la Daily News, Mugini Jacob (kulia) akifanya mahojiano maalumu na Jenerali Musuguri Butiama mkoani Mara. Ilikuwa mwaka 2020 siku ambayo Jenelari Musuguri alikuwa akisherehekea miaka 100 tangu kuzaliwa kwake.
Aprili 2024, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana (kwa sasa ni mstaafu) alifanya ziara mkoani Mara na kupata fursa ya kwenda kumsalimia Jenerali Musuguri nyumbani kwake Butiama. |
Jenerali huyo, ambaye alikuwa na umbo la miraba minne, alikuwa ni kiongozi wa tatu akiwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania akifuata nyayo za Jenerali Mirisho Sam Hagai Sarakikya na Jenerali Abdallah Twalipo, baada ya kutokea mabadiliko ya uongozi jeshini mwaka 1964, ambapo viongozi wazalendo walishika nafasi za juu.
Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda, makamanda wastaafu, askari, marafiki, na Watanzania wote kufuatia kifo cha Jenerali Musuguri.
Rais Samia amemwelezea Jenerali Musuguri kuwa alikuwa mtu shujaa, mwalimu, mshauri na kiongozi aliyeitumikia nchi kwa weledi, umahiri, kujituma, ushujaa na nidhamu.
“Ametuachia mfano bora wa utumishi wa umma utakaoendelea kuwa mwanga ndani na nje ya majeshi yetu,” Rais amesema katika salamu zake jana kupotia ukurasa wake mtandaoni.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>NECTA yatangaza matokeo ya darasa la saba 2024
>>Kura za maoni CCM: Mgombea alia kuhujumiwa kura Tarime Vijijini, akusudia kushitaki kwa Dkt Nchimbi
>>MAKALA:Mwenyekiti Halmashauri Tarime Vijijini ataja miradi ya bilioni 9/- za CSR Barrick North Mara
>>MAKALA MAALUMU:Ajenda ya nishati safi ya kupikia na ugumu wa biashara ya mkaa mjini Bukoba
No comments:
Post a Comment