NEWS

Sunday, 27 October 2024

Mwenyekiti Halmashauri Tarime Vijijini ataja miradi ya bilioni 9/- za CSR Barrick North Mara



Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles.
----------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu

Huenda tatizo la upungufu wa madawati na viti vya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) likabaki historia baada ya samani hizo kupewa kipaumbele kwenye miradi inayotekelezwa kutokana na fedha za CSR kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Utekelezaji wa miradi 101 ambayo itagharimu shilingi bilioni tisa za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), ikiwemo utengenezaji wa madawati hayo tayari umeanza, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Simion Kiles maarufu kwa jina la K.

“Miradi imetangazwa na kuwekwa kwenye mfumo, na utekelezaji unaendelea,” Kiles ameiambia Mara Online News mjini Tarime leo Jumapili.

Amesisitiza kuwa suala la madawati, viti na meza kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari limepewa umuhimu mkubwa.

“Tunatengeneza madawa takriban 6,000 kwa shule za msingi, na viti na meza 4,000 kwa shule za sekondari,” amesema Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga kwa tiketi ya chama tawala - CCM.

Amesema fedha hizo za CSR pia zitumika kugharimia ujenzi wa maabara kadhaa katika shule za sekondari. “Maabara tumezipatia umuhimu sana, zipo karibia 10 zitajengwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Kiles, sehemu ya fedha hizo za CRS zimeelekezwa pia kwenye uimarishaji wa huduma za afya, zikiwemo za mama na mtoto katika vituo vya umma.

“Lakini pia, imo miradi ya barabara na maji, na miradi mingine kama vile ujenzi wa stendi ya kisasa katika eneo la Nyamwaga yalipo makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime,” ameongeza Kiles.

Aidha, fedha hizo pia zimeelekezwa kwenye ujenzi wa soko la dhahabu katika mji mdogo wa Nyamongo, jirani na mgodi wa North Mara.

Mji mdogo wa Sirari uliopo mpakani na nchi ya Kenya nao utanufaika na fedha hizo kwa kujengewa dampo la uchafu.

Kiles ameupongeza mgodi wa North Mara kwa kuendelea kutimiza wajibu wake wa kutoa fedha za CSR kwa wakati na bila ukiritimba.

“Mgodi wa North Mara unatupatia ushirikiano mzuri sana, hauna tatizo lolote,” amesema Mwenyekiti huyo wa Halmashuri ya Wilaya ya Tarime.

Mgodi huo ulitenga shilingi bilioni tisa hivi karibuni kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii katika halmashauri hiyo.

Awamu iliyopita, mgodi huo ulitumia shilingi zaidi ya bilioni saba kugharimia utekelezaji wa miradi mingi ya kijamii kupitia mpango wake wa CSR.

Mbali na CSR, mgodi huo pia unalipa tozo mbalimbali kwa halmashuari hiyo na baadhi ya vijiji. Tozo hizo ni pamoja na ushuru wa huduma (servicey levy) na mirahaba.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages