Mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga akionesha fedha zilizotolewa na wadau wa maendeleo kwaajili ya kununua vifaa vya kujikinga na maambukuzi ya virusi vya corona wilayani hapo. |
Mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga amepokea msaada wa mashine nne (4) za kupumulia kutoka kituo cha afya Songambele kinachomilikiwa na mtu binafsi ikiwa ni mwendelezo wa wilaya kujiweka tayari kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.
Mbali na mchango huo pia amepokea kiasi cha shilingi milioni 5.1 kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wilayani hapo ambazo zitasaidia ununuzi wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mashine hizo kwa mkuu wa wilaya hiyo mganga mkuu wa kituo cha afya cha Songambele kilichopo katika kata ya Nkololo wilayani hapo Dkt. Hellena Sindano amesema wameamua kutoa mashine hizo kwa matumizi ya muda katika kipindi hiki cha maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona .
Aidha Dkt. Sindano ameongeza kuwa tayari kituoni wameweka kifaa maalum cha kisasa kinachoweza kupima joto la mwili pasipo kumgusa wala kumsogelea mtu.
"katika kipindi hiki cha maambukizi ya ugonjwa wa corona kituo cha afya cha Songambele tumeamua kutoa mashine 4 za kupumulia ambazo zitamsaidia mtu mwenye shida ya upumuaji na lengo ni kukabiliana na ueneaji wa maambukizi ugonjwa huu" Alisema Dkt Sindano
Nao waganga wakuu akiwemo Dkt. Judith Ringia wa halmashauri ya mji wa Bariadi na Dkt. Joseph Mziba kutoka wilaya ya Bariadi wamewashukuru wadau hao huku wakitoa rai kwa wadau hao na wengine zoezi hilo lisiishie siku moja na badala yake liwe zoezi endelevu mpaka ugonjwa utakapoisha .
Kwa upande wao wadau wamesema wameamua kuunga jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani ugonjwa huo unagusa jamii nzima ya Watanzania na dunia kwa ujumla.
(Habari na Anita Balingilaki, Bariadi)
No comments:
Post a Comment