MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wadau wote watakaokwenda kupata huduma katika ofisi zake nchini kuanzia leo Jumatatu Aprili 20 na kuendelea kuhakikisha wamevaa barakoa ili kujikinga wenyewe na kuwakinga wenzao dhidi ya maambukizi mapya ya virusi vya corona (COVID-19) vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
Taarifa ya TRA iliyotolewa kwa umma kupitia idara ya huduma na elimu kwa mlipakodi makao makuu leo Jumapili Aprili 19, 2020, imesema hatua hiyo ni kufuatia maelekezo ya serikali kutaka kila mtu kuchukua hatua za kujikinga na kuzuia maambukizi mapya nchini.
Pia walipakodi watatakiwa kuzingatia maelekezo ya kujikinga na kuwakinga wengine kama inavyoelekezwa na wizara yenye dhamana ya afya mara kwa mara ikiwemo kunawa mikono na kupaka vitakasa mikono wakati wa kuingia na kutoka katika ofisi za mamlaka hiyo.
Hata hivyo, ili kuzuia msongamano, TRA kupitia taarifa hiyo imewahimiza walipakodi na wadau wengine kutumia njia mbadala za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kupiga simu bila malipo (0800-750075 au 0800-780078), kutuma ujumbe wa WhatsApp (0744-233333), barua pepe (huduma@tra.go.tz) na kutembelea tovuti yake (www.tra.go.tz) kupata baadhi ya huduma zake.
No comments:
Post a Comment