NEWS

Saturday 18 April 2020

Watu 34 waruhusiwa karantini mkoani Simiyu


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka 

WATU 34 waliokuwa wamewekwa karantini mkoani Simiyu wameruhusiwa kuondoka, hivyo kufanya idadi kupungua kutoka 102 waliokuwepo hadi 68.

Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka, amesema watu hao 34 wameruhusiwa kutoka karantini leo Aprili 18, 2020 baada ya kukaa huko siku 14 na vipimo walivyochukuliwa kuonesha hawana maambukizi ya virusi vya corona (COVID-19.

 Mtaka amesema waliopo karantini ni Watanzania waliotoka nchi zenye maambukizi na kwamba wengi wao waliomba wenyewe kujitenga bila kushurutishwa.

RC Mtaka ( kushoto mwenye shati akiwa kwenye maombi na waumini wengine)
Kwa mujibu wa Mtaka, hadi sasa mkoa wa Simiyu hauna mtu mwenye maambukizi ya virusi vya corona.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amewataka wazazi na walezi kuweka ratiba za wanafunzi kujisomea nyumbani kipindi hiki ambacho shule zimefungwa kupisha mapambano dhidi ya janga hilo la kimataifa.

Mtaka ameyasema hayo leo Aprili 18, 2020 wakati akiongea na waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato mjini Bariadi na kusisitiza kuwa mwanafunzi lazima atengewe muda wa kujisomea hata kama anawasaidia wazazi shughuli za nyumbani.
Baadhi ya waumini wa SDA  wakiwa kwenye ibaada ya jumamosi 

kwa upande wake, Mchungaji Marco Mligwa wa kanisa hilo mtaa wa Ntuzu, amemshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kutenga siku tatu za kufanya maombi kwa Mungu ili aliondolee taifa mlipuko wa ugonjwa hatari wa COVID-19.

Nao waumini wa kanisa hilo akiwemo Mhandisi Paul Jidayi, Mariam Manyangu na Eunice Matondo, wameipongeza serikali kwa jitihada inazofanya katika kukabiliana na janga hilo.

(Na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages