NEWS

Friday 24 April 2020

Diwani Busega abuni barakoa za soksi

 
KATIKA juhudi za kukabiliana na janga la corona, Diwani wa Kata ya Nyashimo iliyopo wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Mickness Mahela, amebuni mbinu mbadala ya barakoa.

Mahela amesema wananchi waweza kutumia soksi na tissue paper kutengeneza barakoa inayofuliwa na kupigwa pasi kwa ajili ya kujikinga na kuwakinga wengine dhiri ya ugonjwa huo.

“Kwa hapa kwetu [Busega] pea moja ya soksi inapatikana kwa shilingi 1,000 japo maeneo mengine zinapatikana kwa shilingi 500 na kwenye pea moja unapata barakoa mbili,” amesema Mahela na kuongeza:

“Huna haja ya kuingia gharama ya lastiki, ukishakata soksi yako mwanzoni na mwishoni unatoboa sehemu ambayo itakusaidia kuweka kwenye masikio ili barakoa yako ikae vizuri na katikati unaweka tissue, kikubwa hapa ikate kwa umaridadi iwe na muonekano mzuri.”

 Diwani wa Kata ya Nyashimo, Mickeness Mahela,(Mwenye nguo ya kijani )akiwa na baadhi ya wananchi aliowapatia elimu ya kutengeneza barakoa za soksi.

Aidha, diwani huyo amesema mbali ya kuifua barakoa hiyo lazima tissue paper iliyowekwa katikati ibadilishwe mara kwa mara.

Tayari diwani huyo ameshatoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya bodaboda juu ya kutengeneza na kutumia barakoa hizo.

Wakizungumza na Mara Online kwa nyakati tofauti wilayani Busega, baadhi ya wananchi waliopewa elimu hiyo wametoa shukrani zao kwa diwani huyu kwa ubunifu huo na kuonesha moyo wa kujali afya za wananchi kipindi hiki cha mapambano dhidi ya corona.

“Tunamshuru mheshimiwa diwani kwa elimu hii, kwa kweli ameonesha moyo wa kipekee kwetu na ukiangalia barakoa hizi hazina gharama kubwa, hata mwananchi wa chini anaweza kumudu gharama,” amesema Maduhu Kwirasa.
          (Habari na Anita Balingilaki, Busega)


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages