NEWS

Thursday 30 April 2020

Vivutio vya utalii, fahari ya Kanda ya Ziwa


KANDA ya Ziwa imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali zikiwemo Hifadhi za Taifa za Serengeti, Rubondo, Saanane na Burigi-Chato.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa upande wa Kanda ya Ziwa inapakana na mikoa ya Mara na Simiyu. Inaaminika ndiyo eneo la kwanza duniani linalotambulika kama urithi wa dunia na hifadhi ya mazingira hai (Biosphere Reserve).




Ndiyo hifadhi pekee duniani yenye makundi makubwa ya wanyama wahamao na idadi kubwa ya wanyama walao nyama, nyasi na majani.

Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Serengeti ni miongoni mwa hifadhi za zamani sana barani Afrika na kituo muhimu cha ndege wa asili na wahamao kutoka nchi za Kaskazini mwa dunia.

Mwaka 2015 hifadhi hii ilitangazwa na mtandao maarufu wa kimataifa unaojulikana kwa jina la ‘Safaris Bookings’ kwamba ndiyo inayoongoza kwa kuwa na vivutio bora vya utalii barani Afrika.

Kamishina wa Uhifadhi Tanapa, Allan Kijazi anasema uteuzi huo ulifanyika baada ya hifadhi hii kushindanishwa na hifadhi nyingine 50 barani Afrika zikiwemo za Afrika Kusini.

Wanyama wanaoipendezesha zaidi hifadhi hii ya Serengeti ni nyumbu na pundamilia wenye historia ya kipekee. Ukifika hifadhini utawaona wakiwa katika makundi makubwa na misafara mirefu wakitafuta malisho na kufurahia mazingira hai.

Mwongoza watalii katika hifadhi hii, Julius Muhale kutoka kampuni ijulikanayo kama Serengeti Services, anasema watalii wengi hupendelea kupelekwa maeneo yenye makundi na misafara ya nyumbu na pundamilia.


Mmoja wa watalii wa ndani aliyezuru hifadhi hii ya Serengeti hivi karibuni, Pinner Kiwia anaelezea kuvutiwa kwake na wanyama hao, miongoni mwa wengine.

“Nimeona wanyama wengi lakini walionivutia zaidi ni nyumbu na pundamilia. Ninatamani kurudi tena kufurahia vivutio vya utalii katika hifadhi hii,” anasema Kiwia.

Mkoani Mwanza kuna Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane. Hii nayo ina utajiri wa vivutio lukuki vya utalii ambavyo ni pamoja na wanyama kama swala pala, fisi maji, mamba, pimbi, tumbili na kobe. Pia ndege wazuri wa aina nyingi na nyoka wakiwemo chatu.
Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane
Upekee wa hifadhi hii ambayo ni kisiwa katika Ziwa Victoria, ni pamoja na uwepo wa wanyama aina ya ‘de brazas monkey’ wasiopatikana sehemu nyingine Tanzania.

Unapokuwa ndani ya hifadhi hii pia unapata fursa ya kuona mandhari nzuri ya asili yenye miamba mikubwa, vichaka, miti na nyasi fupi, fukwe na uwanda mwanana wa Ziwa Victoria.

Mkoani Geita kuna Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo. Hifadhi hii ni makazi na mazingira muafaka ya kuzaliana kwa samaki wakiwemo sato na sangara.

Pia hifadhi hii ni maskani makuu ya ndege wala samaki kama zumbuli (kingfisher), chechele (flycatcher) na taisamaki (fish eagle).

Mbali ya ndege hao, kisiwa hiki ni makazi ya aina nyingine nyingi za ndege wa majini na mimea mbalimbali inayotoa harufa nzuri.

Baadhi ya anyama wakazi wa hifadhi hii ya Rubondo ni viboko, pongo, nzohe, fisi maji, mamba na pimbi wanaoshirikiana makazi na wanyama waliohamishiwa katika hifadhi hii kama sokwe, tembo, twiga, mbega weusi na weupe.

Sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo
Kwa upande wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato iliyotokana na kuunganishwa kwa mapori ya akiba ya Kimisi, Burigi na Biharamulo, inaendelea kuwa maarufu kwa wanyama wanaohamishiwa humo kutoka hifadhi mbalimbali.
Twiga wakifurahia mandhari ya Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato
 Hifadhi hii iliyopo mkoani Geita ilizinduliwa Julai 2019 na Rais Dk John Magufuli ambaye alisema imefanya Tanzania kuwa na eneo la hifadhi za taifa lenye ukubwa wa kilomita za mraba 361,594.

Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, mpango wa wizara hiyo ni kuongeza vivutio vya utalii, hasa wanyama wakiwamo faru kwenye hifadhi hii.
Dkt Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania
Kivutio kingine kikubwa cha utalii katika kanda hii ni Ziwa Victoria lenye ukubwa wa kilomita za mraba 68,800, ambalo ni la kwanza kwa ukubwa Afrika na la pili kwa ukubwa duniani baada ya Superior lililopo Marekani.

Ziwa hili linapakana na mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Geita katika Kanda ya Ziwa. Kwa upande mwingine, limetambaa kuunganisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Linabeba rasilimali za samaki na maji baridi na ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa karibu nchi zote zinazounda Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Kanda ya Ziwa pia kuna Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambao ni sehemu ya vivutio vya utalii katika kanda hii. Uwanja huu una sifa ya kipekee ya kijiografia ya kuwa katikati ya Ukanda wa Maziwa Makuu unaoundwa na nchi 11.

Nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Angola, Sudan na Zambia.

Kwa mujibu wa tovuti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania - TAA (www.taa.go.tz), uwanja huu wa Mwanza ni wa tatu kwa ukubwa wa mindombinu ya kuhudumia ndege za abiria na mizigo na kibiashara hapa nchini baada ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Ziwa Victoria mkoani Mwanza
 Pia kuna Makumbusho ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika wilaya ya Butiama mkoani Mara alikozaliwa na kuzikwa, Makumbusho ya Utamaduni wa Kabila la Wasukuma Bojora na Soko la Kimataifa lenye maduka ya kifahari la Rocky City jijini Mwanza.
Makumbusho ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 

Vivutio vingine vya utalii vilivyopo Kanda ya Ziwa ni daraja la juu la wenda kwa miguu la Furahisha na ghorofa la kwanza kujengwa katika Afrika Mashariki la Nyanza lililopo jijini Mwanza.

Vingine ni bandari, kituo cha reli, makazi ya watu milimani, jiwe lililopo kisiwani Ukerewe mkoani Mwanza linalodaiwa kucheza kila linapoimbiwa wimbo, Mto Mara na chemichemi ya maji ya moto katika kijiji cha Majimoto wilayani Serengeti, Mara.

Utajiri wa vivutio hivi vya utalii utakuwa na maana kama vitatangazwa kikamilifu na kutembelewa na watalii wengi wa ndani na kigeni ili pamoja na manufaa mengine, kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi na taifa kwa jumla.

Mshindi wa Tuzo ya Utalii wa Ndani kwa mwaka 2012 iliyotolewa na Tanapa, Phinias Bashaya anasema kuzuru maeneo yenye vivutio vya utalii kunamwezesha mtu kuona vitu ambavyo havipatikani uraiani.

Mfano, unapotembelea hifadhi za taifa nchini unajionea ikolojia, maisha ya wanyamapori, kujua umuhimu na mchango wake katika maendeleo ya taifa letu,” anaongeza Bashaya.

Mhitimu wa Chuo cha Uhifadhi wa Wanyamapori Mweka kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro, Heriel Masaki, anasema “Ukitembelea maeneo ya vivutio vya utalii unapata nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa kuhusu utalii na uhifadhi.”

Akizungumzia utalii wa ndani, Masaki anasema pia hushawishi wananchi kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi kuepusha uharibifu wa mazingira na migogoro ya kuvamia maeneo ya hifadhi.

Mkazi wa jijini Mwanza, Rehema Mang’era, anasema kuzuru maeneo ya vivutio vya utalii, hususan katika hifadhi za taifa nchini kunambadilisha mtu kisaikolojia, ndiyo maana hata shule za msingi, sekondari na vyuo mbalimbali vinaratibu safari za wanafunzi wao kutembelea hifadhi hizi.

“Kwa hiyo ni vizuri wananchi wote wajenge utamaduni wa kutembelea hifazi za taifa nchini ili kujifunza mambo mengi ya utafiti na kihistoria ya wanyamapori, ndege, wadudu, mimea na mazingira hai. Lakini pia wanasayansi wanasema ukiona maua mazuri na wanyama unaongeza miaka yako ya kuishi duniani,” anasema Mang’era.

Mtaalamu wa tiba za wanyamapori, Dk Titus Kamani anasema kuna umuhimu wa Watanzania kujenga tabia ya kutembelea hifadhi za taifa mara kwa mara ili pamoja na faida nyingine, kupata fursa ya kujua tabia za wanyamapori, miongoni mwa viumbe hai wengine.

Watu wengi hawajui tabia za wanyamapori kwa sababu hawatembelei hifadhi. Wanyama kama sokwe mmoja wao akifa huweka matanga,” anasema Dk Kamani.

Mhifadhi Mkuu wa Tanapa, Kijazi, anaona umuhimu wa shirika hilo na wadau wengine kuongeza kasi ya kuvitangaza vivutio vya utalii nchini vikiwamo hivyo vilivyopo Kanda ya Ziwa ili watu wengi ndani na nje ya nchi wahamasike kuvitembelea.

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ndiyo yenye dhamana ya kuratibu safari za wadau mbalimbali wanaokwenda kutangaza vivutio vya utalii katika maonesho na masoko ya kimataifa.

Msimamizi wa TTB Kanda ya Ziwa, Gloria Munhambo anasema juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk Magufuli za kuwekeza kwenye sekta ya usafiri wa anga kwa kununua ndege za masafa marefu, ni kichocheo cha shughuli za utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo Kanda ya Ziwa na nchini kwa jumla.

Munhambo anatoa wito kwa vyombo vya habari nchini kuunga mkono juhudi za TTB, Wizara ya Maliasili na Utalii na serikali kwa jumla katika kutangaza vivutio hivyo ndani na nje ya nchi ili kushawishi watu wengi kutoka pembe zote duniani kuvitembelea.

Matarajio yake ni kwamba utangazaji wa vivutio vya utalii nchini utaendelea kufanyika kwa umakini unaozingatia kulinda maslahi ya taifa ili kuepusha hali yoyote inayoweza kukwaza watalii wa ndani na kigeni wenye nia ya kuzuru maeneo yanayovihifadhi.
 
(Imeandikwa na Christopher Gamaina)

1 comment:

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages