KATIKA
kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu nchini, wanasiasa wengi wameona umuhimu
wa kuweka wazi ajenda na matamanio yao juu ya maendeleo ya wananchi.
Miongoni
mwao ni kijana msomi na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nikodemus Kerarya
maarufu zaidi kwa jina la Nico, mkazi wa jimbo la Tarime Vijijini.
Nico akizungumza katika hafla ya kuchangia vikundi vya maendeleo |
Katika
mahojiano maalumu na gazeti la Sauti ya Mara hivi karibuni, Nico ameweka bayana ajenda yake kuu kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi mkuu kuwa ni kuona Tarime Vijijini ikistawi kwa uchumi wenye tija kwa
wakazi wake.
Yafuatayo
ndio mahojiano yenyewe:
Sauti ya Mara: Ndugu Nico,
wewe ni kijana ambaye umekuwa na mitazamo chanya katika masuala ya maendeleo ya
wananchi. Una ajenda gani ya msisimko wa kimaendeleo kipindi hiki cha kuelekea
uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani nchini?
Nico: Ajenda yangu kuu
na muhimu kipindi hiki ni Tarime Vijijini yenye uchumi wenye tija wananchi.
Tarime
ni wilaya iliyojaaliwa kuwa na rasilimali nyingi za uchumi. Hata hivyo,
tunapaswa kuzitambua fursa za uchumi kwa tija ya maendeleo yetu.
Nico akikagua miradi ambayo inaweza kuwakomboa vijana |
Tarime
Vijijini tunahitaji viwanda, hii ni kwa sababu zipo fursa za kilimo, mazao yote
yanakubalika huku.
Pia
zipo fursa za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu. Maeneo mengi Tarime Vijijini yamezungukwa
na madini.
Hivyo,
kama utaratibu wa msingi utafanyika wa kuwatafutia wachimbaji wadogo wadogo
maeneo mbadala ya uchimbaji, kipato cha wananchi kitaongezeka maradufu.
Sauti ya Mara: Ni mambo gani
hasa ambayo unaona bado yanahitaji msukumo zaidi kutoka kwa viongozi
watakaopatikana kupitia uchaguzi mkuu ujao?
Nico: Yapo mambo
mengi ya kiutendaji na uwajibikaji kwa viongozi.
Kwanza,
jamii ya Tarime Vijijini inahitaji maji safi na salama kwa matumizi mbalimbali.
Maeneo
mengi ya jimbo hili yana changamoto kubwa ya maji. Hivyo, kiongozi/viongozi
watakao pata fursa ya kuwakilisha wananchi lazima washughulikie changamoto ya
maji.
Pili,
jimbo letu lina changamoto kubwa ya barabara. Mfano, barabara itokayo Tarime,
Nyamwaga, Nyamongo hadi wilaya ya Serengeti ni muhimu kama kiunganishi cha
wilaya hizi, lakini pia ni njia kuu ya watalii watokao nchini Kenya kuelekea
hifadhi za Serengeti na Ngorongoro.
Zipo
pia barabara nyingi zenye changamoto kubwa lakini ni muhimu kwa uchumi wetu,
hasa katika usafirishaji mazao na mifugo. Watakaopata fursa walishughulikie
hilo.
Tatu,
kuna baadhi ya maeneo yanapaswa kupewa hadhi ya mamlaka ya mji; kama vile mji
wa Nyamongo na Sirari. Suala hili limezembewa, hivyo kuendelea kufifiisha
jitihada za maendeleo katika sehemu hizo.
Nne,
yapo masuala ya huduma za afya. Hili bado ni tatizo, hasa mfumo utumikao sasa
wa kupata dawa katika vituo vyetu vya afya na masuala mengine ya uendeshaji.
Changamoto ya afya ni kubwa kulingana na matarajio ya wengi.
Tano,
ili kuweka kiunganishi cha wakulima na wafanyabiashara, eneo la Sirari
linapaswa kuboreshwa na kuweka soko la kimataifa la mazao.
Kwa
kuwa eneo hilo ni mahususi kama njia kiunganishi ya mikoa mbalimbali, ni vyema
ikawa Center of Collections (kituo cha ukusanyaji) ya mazao ya kilimo na kukuza
uchumi.
Sauti ya Mara: Wewe binafsi
umejipangaje na ushiriki wako wa moja kwa moja katika hayo utakuwaje?
Nico: Suala kubwa
na la msingi kwanza, nimejiandaa kwa kuhakiki taarifa zangu za mpigakura.
Lakini
pia nimejiandaa kushiriki katika uchaguzi, hasa katika nafasi ya kuchagua na
kuchaguliwa. Na kwa kuwa ni haki yangu kikatiba, nitayatimiza yote kwa utashi
wangu na kwa mujibu wa sheria za nchi.
Nico akiwa katika shughuli za ujenzi wa chama(CCM) |
Sauti ya Mara: Kwa muda
mrefu sasa umekuwa msaada kwa vijana wa jinsia zote, hasa katika masuala ya
ujasiriamali na uwezeshwaji. Je, unadhani bado kundi hilo la jamii linahitaji
kupewa kipaumbele katika masuala ya kujikwamua kiuchumi?
Nico: Ndiyo. Kwanza,
ifahamike kuwa vijana ni kundi muhimu linaloweza kuzalisha kwa ziada nchini.
Pia vijana ni kundi lenye wajibu wa kuilinda jamii katika masuala yote ya
kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Hivyo,
kuna haja ya kuendelea kulisaidia kundi hili kwa kuliwezesha kiuchumi. Mfano,
kupewa mikopo yenye riba nafuu au isiyokuwa na riba kabisa, kuliwezesha katika
fikra za uzalishaji mali na uongozi thabiti wa kimkakati na kimaendeleo.
Nico akiwa akihamasisha maendeleo |
Tuna
wajibu wa kuwafanya vijana kuwa sehemu timilifu ya jamii yetu katika nyanja
zote za uwajibikaji.
Sauti ya Mara: Ungependa
kuona vijana wanawezeshwa zaidi katika nyanja gani?
Nico: Kwanza,
mikopo yenye riba nafuu au isiyo na riba. Pili, wapewe na waaminiwe katika
fursa za uongozi na hasa nafasi za uwakilishi wa jamii katika taasisi
mbalimbali. Tatu, washirikishwe katika maamzi mbalimbali yahusuyo maisha ya
jamii yao.
Sauti ya Mara: Tumeona
umekuwa muumuni mzuri wa kuhamasisha vijana kufikiria kuisaidia nchi badala ya
kutaka nchi ndiyo iwasaidie. Je, ni mambo gani makubwa na yenye maslahi mapana
ya umma ambayo wewe kama kijana umeweza kuisaidia nchi kupitia kwa wananchi?
Nico: Ni kweli
nimeshiriki katika hamasa mbalimbali za kimaendeleo katika jamii yangu na hata
kujitolea kwa rasilimali fedha, nguvu na ushawishi ili jamii yangu isonge
mbele. Yapo mambo kadhaa nimeweza kuyafanya.
Nico(kulia) akikabidhi msaada wa mifuko ya Saruji |
Moja,
nimeshiriki katika masuala ya uundwaji wa vikundi mbalimbali vya uzalishaji
mali na kuvisimamia ili vifikie mafanikio. Mfano, ni Jikomboe, Mbuya Honey, Mt.
Anna, Nyada, Nyabibago, kwa kutaja baadhi.
Pia
nimekuwa mwakilishi wa jamii ya Nyamongo katika Mfuko wa Dhamana wa Jamii ya
Mara Kaskazini, nimefanikiwa kuishawishi taasisi hii kupima viwanja (kurasimisha
makazi) zaidi ya 12,000 katika miji ya Nyamongo na Nyamwaga.
Aidha,
nikiwa nafanya kazi katika mgodi wa North Mara, nilifanikiwa kuushawishi
uongozi wa mgodi huo kufanya marekebisho ya miradi mbalimbali ya jamii kupitia
mikataba halisi na jamii, yaani Village
Benefit Agreement - VBA na Village
Benefit Implementation Agreement - VBIA.
Pia
nimefanikiwa kuushawishi uongozi wa mgodi huo kuanzisha tamasha la
wajasiriamali linalosaidia jamii iliyo jirani kuzitambua fursa za maendeleo na
uchumi.
Vilevile,
nilifanikiwa kushawishi uanzishaji wa tamasha la michezo linalosaidia kuibua
vipaji mbalimbali vya vijana na kuwajenga kiafya, kiakili na kujipatia ajira.
Hayo nimetaja baadhi tu miongoni mwa mengi niliyowezesha.
Sauti ya Mara: Je,
unaridhika na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi, hususan katika jimbo la
Tarime Vijijini ambako wewe ni mzaliwa na mkazi wa huko?
Nico: Kwa maana ya
uwajibikaji wa chama changu cha CCM, viongozi wamejitahidi kusaidia hatua
mbalimbali za kutatua migogoro mikubwa ya jamii katika nyanja tofauti.
Serikali
kupitia halmshauri imesaidia katika ujenzi wa miundombinu kulingana na bajeti,
japo jitihada kubwa zinahitajika ili kuiona Tarime Vijijini imebadilika
kiuchumi na kimaendeleo.
Nico anaamini kilimo cha bustani bora kinaweza kukomboa vijana |
Sauti ya Mara: Mwisho
unadhani wapigakura wazingatie vigezo gani kuhakikisha wanatumia haki zao za
kidemokrasia na kikatiba katika kuwapata viongozi watakaowatumikia kwa kiwango
cha kuridhisha?
Nico: Kwanza,
mwakilishi wa wananchi awe ni mtu anaezitambua vyema changamoto za wananchi wa jimbo
la Tarime Vijijini, sio za kuambiwa tu, bali azijue na aziishi katika hatua
mbadala, yaani kwa kuzitafutia ufumbuzi.
Pili,
awe mkazi wa jimbo hili, sio mbeba begi anayetaka uongozi wa tumbo lake na
familia yake binafsi badala ya wananchi kwa jumla.
Tatu,
awe na uwezo mbadala wa kuzitambua fursa za maendeleo na si tu kutegemea
Serikali Kuu.
Nne,
awe na uwezo wa kufanya siasa za maendeleo na si siasa za siasa.
(Imeandikwa na
Christopher Gamaina)
No comments:
Post a Comment