SERIKALI imewahimiza
wakulima wa kahawa mkoani Mara kuchangamkia kilimo hicho kwa kuwa imewajengea
mazingira mazuri ya upatikanaji wa mkopo wa fedha na soko la zao hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime
mkoani Mara, Mhandisi Mtemi Msafiri, ameyasema hayo mjini Tarime juzi, wakati
akifungua mkutano wa Wakulima wa Mara Cooperative Union (WAMACU) Ltd
wanaojishughulisha na kilimo cha kahawa mkoani Mara.
“Kuna kazi kubwa inafanywa
na Serikali katika kufufua mazao ya kimkakati ikiwamo kahawa, na ikumbukwe kuwa
kahawa ya Tanzania inaaminika kwa ubora Afrika Mashariki,” amesema Mhandisi
Msafiri na kuendelea:
“Rais [Dkt John Magufu]
anataka wakulima wanufaike na kilimo, ndio maana Benki ya Maendeleo ya Kilimo
Tanzania (TADB) imeanza kuwakopesha wakulima wa kahawa fedha za uendeshaji kwa
riba nafuu ya asilimia tisa, lakini pia Serikali imepata wanunuzi wa uhakika wa
zao hilo.”
Hata hivyo, mkiuu huyo wa
wilaya amewataka wakulima hao kujenga utamaduni wa kurejesha mikopo ya fedha
kwa wakati ili kuwezesha wengine kukopa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa zao
hilo.
Mapema, Mhandisi Msafiri
amesomewa taarifa ya WAMACU Ltd ambayo imetaja mafanikio ya wakulima hao kuwa
ni pamoja na kupata mkopo wa shilingi bilioni 1.682 kutoka TADB, kupata ofisi
na kuajiri mhasimu na meneja shughuli.
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment