NEWS

Thursday 16 July 2020

Bunda Mjini haikamatiki wawania ubunge Mara


JIMBO la Bunda Mjini huenda likaweka historia ya kuwa na idadi kubwa ya makada wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge mkoani Mara, akiwamo mbunge wa zamani, Stephen Wasira (pichani kushoto).

Hadi kufukia jioni jana Jualai 15, 2020, jimbo hilo lilikuwa linaongoza kwa kuwa na makada wengi waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa na kugombea ubunge ukilinganisha na majimbo mengine mkoani humo, kwa mijibu wa Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Shaibu Ngatiche.

“Hadi jana (Jumatano) jimbo lenye idadi kubwa ni Bunda Mjiini ambapo waliochukua fomu ya  ubunge ni 60,” Ngatiche ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo asubuhi.

Ngatiche amesema jimbo la Musoma Mjini lilikuwa linafuatia Bunda Mjini kwa kuwa na wananchama wa CCM waliochukua fomu 54 likifuatiwa na jimbo la Serengeti (50).

Ametaja majimbo mengine na idadi ya waliokuwa wamechukua fomu ya ubunge ikiwa kwenye mabano kuwa ni Rorya (42), Bunda Vijijini (31), Musoma Vijijini (29), Tarime Vijijini (27) na Tarime Mjini (18).

“Mkoa wetu unaweza kuwa na idadi kubwa ya waliochukua fomu ya ubunge na tunategemea idadi hiyo kuongezeka leo na kesho,” amesema katibu huyo wa CCM.
Shaibu Ngatiche
Aidha, Ngatiche amesema wanachama 44 wa CCM wakiwemo vijana 12 wamejitokeza kuwania ubunge kupitia jumuiya mbalimbali za chama hicho.

“Hadi sasa vijana kupitia UVCCM wapo 12, Wazazi ni mmoja na kupitia UWT ni 31,” amesema Ngatiche.

Katika hali ya kuvutia, maprofesa kadhaa wamejitokeza ‘kunyukana’ na mbunge wa Musoma Vijijini anayemaliza muda wake, Profesa Sospeter Muhongo katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo.

“Waliochukua fomu Musoma Vijijini hadi kufikia jana (Jumatano) ni 29 wakiwemo maprofesa wengi,” amesema Ngatiche.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages