NEWS

Saturday 19 December 2020

Asilimia 93 wanafunzi Simiyu wachaguliwa kidato cha kwanza 2021

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Miriam Mmbaga akitangaza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.

 

WANAFUNZI 27,433 (wavulana 12,751 na wasichana 14,682) mkoani Simiyu wamefaulu Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2020 kwa alama kati ya 100 na 250.


Hata hivyo, wanafunzi 25,596 (wavulana 12,116 na wasichana 13,480) sawa na asilimia 93.3 waliofaulu mtihani huo, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.


Hayo yamesemwa jana Desemba 18, 2020 na Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Miriam Mmbaga wakati akitangaza matokeo ya wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza katika shule za bweni na kutwa mwakani.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho.


Mmbaga ameongeza kuwa wanafunzi 1,837 (wavulana 635 na wasichana 1,202) sawa na asilimia 6.7 ya wanafunzi waliofaulu, hawakuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021 kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa na samani.

Sehemu washiriki wengine wa kikao hicho.

 

"Halmashauri ambazo wanafunzi hawakuchaguliwa ni za wilaya ya Bariadi (wanafunzi 948) Itilima (162) na Meatu (727). Jitihada za haraka zinahitajika ili vyumba vya madarasa na samani vipatikane, hivyo kuwawezesha wanafunzi waliokosa nafasi kuanza kidato cha kwanza kwa chaguo la pili ifikapo Februari 1, 2021,” amesema Mmbaga.

Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Ernest Hinju akiwasilisha taarifa ya uchaguzi wa wananfunzi wa kidato cha kwanza.

 

Awali, akiwasilisha taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2021, Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Ernest Hinju amesema ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 86.46 mwaka 2019 hadi asilimia 91.98 mwaka 2020 - sawa na ongezeko la asilimia 5 .52.

 

Hinju amefafanua  kuwa anafunzi 105 (wavulana 67 na wasichana 38) wamechaguliwa kuingia shule za bweni, 23 (wavulana 16 na wasichana 7) wamechaguliwa kuingia shule za  bweni za mahitaji maalum na 25,464 (wavulana  12,032 na wasichana 13,432) wamechaguliwa kujiunga na shule za kutwa.

Washiriki wengine kikaoni.

 

Katika hatua nyingine, Hinju amesema watahiniwa 417 kutoka shule 11 walifutiwa matokeo kutokana na sababu za udanganyifu, huku akitaja halmashauri husika kuwa ni Wilaya ya Bariadi (shule 9), Bariadi Mji (shule moja) na Wilaya ya Itilima (shule moja).

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Paul Maige akichangia ajenda ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.


Kwa upande wao, wenyeviti wa halmashauri akiwemo Paul Maige kutoka Maswa na Daudi Nyalamu kutoka Itilima, wamesema kupitia vikao vya vya madiwani na watendaji wa serikali wameanza kuchukua hatua za ukamilishaji wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi waweze kupata sehemu ya kusomea.

 

"Kwenye halmashari yetu tumeshaanza mikakati na hatua mbalimbali za kuhakikisha watoto wetu waliofaulu na kukosa sehemu ya kusomea wanaingia shule ifikapo Feburuari na hata leo wakati nakuja Bariadi nimeacha kikao kinaendelea ambacho yupo Mheshimiwa Mbunge na watendaji, na moja ya vitu vitakavyojadiliwa ni pamoja na madarasa,” amesema Nyalamu.

 

Mkoa wa Simiyu una mahitaji ya vyumba vya madarasa 565, vilivyopo ni 419, huku upungufu ukiwa vyumba 155 vinavyohitaka kwa ajili ya kidato cha kwanza mwakani.

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages