NEWS

Thursday 15 July 2021

Wanafunzi 600 hawana choo mwaka mzima Rorya, RC Hapi ampa DED siku 30 kujenga




WANAFUNZI zaidi ya 600 katika Shule ya Sekondari ya Katuru, inayomilikiwa na serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara, hawana choo kwa takriban mwaka mmoja sasa, imethibitika.

Kutokana na ‘aibu’ hiyo, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Salum Hapi leo Julai 15, 2021 amempa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya (DED) hiyo, Charles Chacha Kitamuru muda wa siku 30 kuhakikisha wanafunzi hao wanajengewa choo.

“Nawapa mwezi moja kuanzisa leo wanafunzi wapate matundu ya kujisitiri,” RC Hapi ameagiza wakati alipofanya ziara ya kwanza ya kikazi wilayani Rorya katika mji wa Shirati, leo na kuwapa wananchi nafasi ya kueleza kero zao.



RC Hapi amemtaka DED Kitamuru kutoa maelezo ni kwanini shule hiyo imekosa huduma ya choo cha wanafunzi kwa muda mrefu.
 
Kitamuru amejitetea kwamba halmashauri yake ipo kwenye mchakato wa kugharimia ujenzi wa choo cha wanafunzi katika shule hiyo yenye wanafunzi wa kike na kiume zaidi ya 600.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tumeandaa shilingi milion tatu kwa ajili dharura na zipo tayari,” DED Kitamuru amemueleza RC Hapi.

Mara Online News imefika katika Shule ya Sekondari ya Katuru na kushuhudia choo cha muda kinachotumiwa na wanafunzi, kikiwa kimejengwa kienyeji kwa miti, bila mlango wala paa.

Choo cha muda kinachotumiwa na mamia ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Katuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, kama kilivyokutwa na camera ya Mara Online News, leo mchana.

Mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Musa Mbogo, amemwambia Mkuu huyo wa mkoa kwamba ukosefu wa choo unawalazimu wanafunzi wengi wa shule hiyo kujisaidia vichakani.

Mapema leo asubuhi, RC Hapi amekagua maendeleo ya mradi wa maji wa mji wa Shirati, ambao umeanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa maelfu ya wananchi katika mitaa yote ya mji huo, ambapo amewataka wananchi kulinda miundombinu ya maji, kwani inaigharimu serikali fedha nyingi.

Baadaye, RC Hapi ameendelea na ziara yake ya kikazi katika wilaya jirani ya Tarime, akiwa amefuatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Namba Tatu).


RC Hapi (kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Issa Chikoka (kushoto) wakati alipofanya ziara wilayani humo leo. Katikati ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Namba Tatu.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages