
Kamishna wa TANAPA, Musa Juma Kuji (mwenye shati la mistari myekundu) na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dkt Tutindaga George (kulia kwa Kuji) wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa na askari wa shirika hilo katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane jijini Mwanza jana.
----------------------------------------
Maafisa na askari wa Hifadhi za Taifa nchini wamekumbushwa kuzingatia nidhamu, uadilifu na juhudi katika ulinzi na utunzaji wa raslimali za taifa.
Wito huo ulitolewa na Kamishna wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Musa Juma Kuji wakati akizungumza na maafisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane jijini Mwanza jana.
Kamishna Kuji alisema maafisa na askari wote ni wawakilishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amewaamini na kuwakabidhi jukumu muhimu la ulinzi na utunzaji wa raslimali za taifa kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo.
“Niwahimize tuendelee kuchapa kazi kama ilivyo jadi yetu TANAPA,” alisema Kuji ambaye alikuwa safarini kuelekea Hifadhi ya Ibanda iliyopo wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.
Kiongozi huyo alitumia fursa hiyo pia kumpongeza Askari wa Uhifadhi Daraja la Kwanza, Alpha Jacob Marcel kwa uokozi wa mali za shirika wakati wa tukio la moto katika moja ya majengo ya Hifadhi ya Saanane.
Alibainisha kuwa TANAPA inatambua ushujaa aliouonesha askari huyo shupavu kwa kujitoa mhanga kutetea mali ya shirika hilo.
Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi TANAPA, Dkt Tutindaga George ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, alimsifu Kamishna Kuji kwa kutenga muda wake kutembelea hifadhi hiyo ili kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment