Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele akikabidhi vyeti kwa walimu wa shule zilizofanya vizuri kitaaluma kwa mwaka 2023 wakati wa maadhimisho ya kilele cha Juma la Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) yaliyofanyika jana Septemba 23, 2024.
---------------------------------------
Tarime
Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), mkoani Mara imeadhimisha kilele cha Juma la Elimu na kutunuku vyeti kwa shule zilizofanya vizuri kitaaluma kwa mwaka 2023.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Keryoba iliyopo kata ya Sirari jana Septemba 23, 2024 na kuhusisha pia upandaji miti na michezo mbalimbali.
Yaliyolenga kufanya tathmini ya mambo yanayohusu elimu ya watu wazima, elimu nje ya mfumo rasmi na elimu jumuishi katika shule za awali, msingi, sekondari na vituo vya elimu ya watu wazima na nje ya mfumo rasmi.
Kikundi cha ngoma ya asili kikitumbuiza katika maadhimisho hayo.
-----------------------------------------
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele ambaye aliagiza Afisa Elimu wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalum wanapata elimu.
"Tujitahidi wale watoto ambao wamekosa elimu, wakiwemo wenye mahitaji maalum kuwaleta na kuwaingiza kwenye mfumo wa elimu," alisema DC Gowele.
Pia, kiogozi huyo wa wilaya aliitaka halmashauri hiyo kutumia sehemu ya mapato yake ya ndani kutatua changamoto za kielimu.
"Nisingependa kuona wilaya ya Tarime ikiwa ya mwisho kitaaluma, tutumie mapato yake ya ndani kutatua changamoto za kielimu pamoja na kuwa- motivate (kuwapa motisha) walimu wanaojitolea kufundisha wanafunzi wa MEMKWA," alisema.
DC Gowele akipanda mti wakati wa maadhimisho hayo. Mwenye suruali ya bluu kulia ni Afisa Elimu ya Watu Wazima wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Marina Ngailo
------------------------------------------
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Keryoba, Stanley Stanley alisema maadhimisho hayo ni muhimu kwa sababu yanaikumbusha jamii, wazazi, walezi na walimu kuwa elimu ni haki ya kila mtoto - bila kujali hali aliyonayo.
Naye mwanafunzi wa shule hiyo, Victoria Chacha alisema "Maadhimisho haya yahamasisha wanafunzi kusoma. Tunaomba serikali iwachukulie hatua za kisheria wazazi wanaokatisha wanafunzi masomo."
No comments:
Post a Comment