
Wachezaji wa Kewanja FC wakifurahia kombe la ubingwa wa mashindano ya Mahusiano Cup kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe jana Jumapili.
-------------------------------------------
-------------------------------------
TIMU ya Kewanja FC katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Mahusiano Cup ya mwaka huu wa 2024, ikiwa ni mara yake ya tano mfululizo kushinda kombe hilo.
Kewanja iliibuka na ubingwa huo jana Jumapili baada ya kuichapa Nyamwaga kwa penalti 3-1 katika fainali ya kibabe iliyochezwa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo Nyamongo, kilomita chache kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara unaodhamini mashindano hayo.
Wachezaji wa Kewanja FC
wakifurahia kupokea zawadi.
-----------------------------------------
Mgeni rasmi katika fainali hiyo, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Flowin Gowele aliikabidhi Kewanja FC kombe la ubingwa wa Mahusiano Cup 2024, mbele ya Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, miongoni mwa viongozi wengine.
DC Gowele aliipongeza Barrick North Mara kwa kuanzisha na kudhamini mashindano hayo, huku akiahidi kwamba serikali itaendelea kuipa ushirikiano katika kuyaendeleza, ili kuboresha zaidi uhusiano na jamii inayozunguka mgodi huo.
DC Gowele (katikati) akizungumza mara baada ya kukabidhi kombe kwa Kewanja FC. Wa pili kulia ni GM Lyambiko, Katibu wa Mbunge wa Tarime Vijijini, Remmy Mkapa (wa pili kushoto), Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi (kushoto) na Diwani wa Kata ya Kemambo, Bogomba Richard (kulia).
---------------------------------------------
“Michezo ni afya, burudani, ajira, upendo na ushirikiano. Sisi serikali tunaamini katika uhusiano mzuri na uwekezaji wenye tija kwa pande zote mbili [jamii na mgodi],” alisema kiongozi huyo.
Alisema uendelevu wa mashindano hayo utasaidia kuibua vipaji na kubadilisha mitazamo hasi ya baadhi ya vijana dhidi ya mgodi huo, hivyo kujiepusha na vitendo vya kuuvamia, kupora mawe ya dhahabu na kuharibu miundombinu yake.
DC Goweke na viongozi wa mgodi wa Barrick North Mara wakiwa katika picha ya pamoja timu ya Nyamwaga FC iliyoshika nafasi ya pili katika mashindano hayo.
--------------------------------------------
Awali, GM Lyambiko alisema Barrick North Mara inatumia mashindano hayo kama sehemu ya kuimarisha zaidi uhusiano kati ya mgodi huo na jamii inayouzunguka, sambamba na kujadili changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Alisema Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Dkt Mark Bristow alishaahidi kugharimia ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo katika mji wa Nyamongo, ili kuhamasisha zaidi michezo katika maeneo yanayozungu mgodi huo.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Barrick Gold kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Mashabiki wakishangilia ubingwa wa Kewanja FC kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Ingwe jana jioni.
No comments:
Post a Comment