Nyambari Nyangwine (mwenye suti na kofia), Askofu Michael Msonganzila (kulia kwa Nyambari) na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (wa nne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na masista kadhaa katika Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga jana Jumapili.
------------------------------------------
Tarime
Mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, Nyambari Nyangwine, kwa mara nyingine amechangisha shilingi milioni 224.5 kusaidia ujenzi wa jengo la Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga iliyopo wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Katika mchango huo ambao umehusisha fedha taslimu shilingi milioni 78.9 na vifaa mbalimbali vya ujenzi, Nyangwine amechangia shilingi milioni 27 taslimu.
Nyangwine ambaye alikuwa mgeni rasmi katika harambee ya ujenzi huo kanisani hapo jana Jumapili, pia alichangia vitabu vyenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa ajili ya shule ya kanisa hilo.
Hiyo ni mara ya pili kwa Nyangwine kushiriki katika harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la kanisa hilo kwani Desemba mwaka jana alishiriki na kuchangisha zaidi ya shilingi milioni 200, huku mwenyewe akichangia shilingi milioni 20 taslimu.
“Hii ni mara ya pili na kuwa hapa, na katika harambee hii nimetoa mchango wa shilingi ya milioni 27 na vitabu vya shilingi milioni 15, hivyo mchango wangu katika hii awamu ya pili unakuwa shilingi milioni 42,”, alisema Nyangwine ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime kupitia chama tawala - CCM.
Alitumia fursa hiyo pia kuwahimiza wakazi wa Tarime kuwekeza katika elimu kwa kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya elimu ya msingi hadi chuo kikuu.
“Somesheni watoto, na wasome hadi vyuo vikuu, wasisubiri kuajiriwa, wajiajiri wenyewe kwani hata somo la maadili na ujasiriamali limehimizwa kwenye mitaala mipya,“ alisistiza mfanyabiashara huyo maarufu na mmoja wa wasomi wa vijana nchini.
Nyambari Nyangwine akizungumza
wakati wa harambee hiyo.
----------------------------------------
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele alimshukuru Nyangwine kwa kuitikia mwaliko wa kuwa mgeni ramsi katika harambee ya kupiga jeki ujenzi wa jengo la kanisa hilo.
“Hili ni jambo la maendeleo na tuendelee kudumisha amani na kuwa kitu kimoja,“ alisema DC Gowele ambaye pia alichangia shilingi milioni moja katika harambee hiyo.
Wakati huo huo, Kanisa la Katoliki Parokia ya Nyamgwa imemzawadia Askofu wa Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila gari jipya aina ya Alphad lenye namba za usajili T 805 EJE.
Askofu huyo aliwashukuru wote waliochangia na zawadi nyingine yingi alizopewa liwemo gari hilo na ng’ombe.
Parokia hiyo pia ilimkabidhi Nyangwine zawadi ya ng’ombe wa maziwa kutambua mchango wake wa maendeleo ya kanisa hilo.
Nyambari Nyangwine (mwenye kofia) akipokewa kwa shangwe alipowasili katika viwanja vya Kanisa Katoliki Parokia ya Nyamwaga.
No comments:
Post a Comment