
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati waliokaa) kwenye picha ya pamoja na wanafunzi na viongozi wao walio kwenye msafara wa kwenda nchini Ujerumani.
-------------------------------------------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewaaga rasmi wanafunzi 12 wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Kituo cha Mkoa wa Mara wanaokwenda nchini Ujerumani kwa ziara ya mafunzo ya miezi miwili.
Kabla ya tukio la kuagana Ijumaa iliyopita mjini Musoma, RC Mtambi alifanya kikao kifupi na wanafunzi hao pamoja na viongozi wa safari hiyo.
Wanafunzi hao wa Kituo cha Mkoa wa Mara wamekuwa wa kwanza kutoka OUT kupata fursa hiyo ya kwenda katika Chuo Kikuu cha Ludwig Maximilian, nchini Ujerumani wakiongozwa na Dkt Asha Katamba (Mkurugenzi wa OUT Tanzania - Kituo cha Mkoa wa Mara), Mwalimu Judith Mrimi (Afisa Elimu, Elimu Maalum Mkoa wa Mara) na Dkt Maulid Maulid (Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Wakala wa Uongozi wa Elimu (ADEM).
Wanafunzi hao pamoja na viongozi hao watakwenda Ujerumani kwa lengo la kubadilishana ujuzi, uzoefu na maarifa ya kusaidia suala la ufundishaji na ujifunzaji wa elimu jumuishi na ujasiriamali katika shule za msingi na sekondari za mkoani Mara.
Aidha, RC Mtambi aliwatakia wanafunzi na viongozi wao safari njema ya kuelekea nchini Ujerumani huku akiwakumbusha kuwa mabalozi wazuri wa nchi ya Tanzania na kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Tanzania.
Pia, aliwataka kutumia fursa hiyo kujifunza na kupata maarifa, ujuzi na uzoefu utakaosaidia kuboresha elimu jumuishi katika mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, kiongozi huyo wa mkoa alipongeza ushirikiano uliopo kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Ludwig Maximilian kilichopo mjini Munich, nchini Ujerumani.
Ziara hiyo ya wanafunzi na viongozi wao imetokana na ufadhili wa Taasisi ya ERASMUS+ ya Ulaya ambao ni wa miaka mitatu kuanzia mwaka huu.
Kupitia ufadhili huo wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania - Kituo cha Mkoa wa Mara wataweza kwenda kwa zamu nchini Ujerumani kwa miaka mitatu mfululizo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Waziri Simbachawene aanza ziara ya kikazi mkoani Mara
>>Nyambari achangisha tena shilingi zaidi ya milioni 200 Kanisa Katoliki Nyamwaga, mwenyewe achangia milioni 42/-, Parokia yamkabidhi Askofu Msonganzila gari jipya
>>SpaceX arrives at the space station to rescue stranded astronauts
>>Mradi wa Smart City wayeyuka Serengeti, ni ule uliotangazwa kutengewa shilingi trilioni 2
No comments:
Post a Comment