NEWS

Monday, 23 September 2024

Serikali yaipa RUWASA Mara magari mapya





Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (Katikati) akikata utepe mjini Musoma wiki iliyopita katika hafla ya kuikabidhi RUWASA magari mawili mapya yaliyotolewa na serikali. Kushoto ni Katibu Tawala Mkoa huo, Gerald Musabila Kusaya na wa pili kutoka kulia ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mara, Mhandisi Tulimpoki Mwakalukwa.


Na mwandishi wetu,Musoma
-----------------------------------

Serikali imeipatia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara magari mawili mapya yatakayotumika katika wilaya za Tarime na Serengeti.
Hafla ya kuyakabidhi iliongozwa na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi mjini Musoma wiki iliyopita, ambapo aliwataka watendaji wa RUWASA waliopata magari hayo kuhakikisha yanatumika vizuri na kuwaongezea kasi ya kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.

“Ni matumaini yangu kuwa magari haya yatatumika kuboresha huduma za upatikanaji wa maji kwa wananchi,” alisema RC Mtambi.

Pia, aliwataka wakuu wa wilaya kufuatilia kwa karibu matumizi sahihi ya magari hayo ili yadumu muda mrefu kwa ajili ya kuwapatia wananchi huduma bora ya maji.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mara, Mhandisi Tulimpoki Mwakalukwa aliishukuru serikali kwa kutoa magari hayo akisema walikuwa wanayahitaji kama vitendea kazi muhimu.

Mhandishi Mwakalukwa alibainisha kuwa magari hayo yameongeza idadi ya waliyonayo kutoka matatu hadi matano, yakiwemo mawili yaliyogawiwa kwa ofisi za RUWASA wilaya za Butiama na Bunda.

Kwa mujibu wa meneja huyo, kwa sasa ofisi za RUWASA mkoani Mara ambazo hazina magari ni za wilaya za Musoma na Rorya, ambazo hata hivyo alisema zimeshaombewa magari serikalini.

Mhandisi Mwakalukwa alitumia nafasi hiyo pia kumshukuru Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa kuidhinisha ununuzi na kuugawia mkoa wa Mara magari hayo ambayo ameahidi kusimamia kwa karibu matumizi yake.

Naye Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Malando Masheku aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia ofisi yake kitendea kazi muhimu.

Mhandisi Mashepu alisema gari hilo litaisaidia ofisi yake katika kuwafikia wananchi na kuwatatulia changamoto za huduma ya maji kwa wakati.

RUWASA ilianzishwa nchini Tanzania chini ya Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya Mwaka 2019, ili kuongeza, kuboresha na kuwezesha huduma za maji na usafi wa mazingira kwa wananchi vijijini kuwa endelevu.

Majukumu ya RUWASA ni pamoja na kusanifu, kujenga na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji na uendeshaji wake kupitia vyombo vya kijamii.

Mengine ni kuvijengewa uwezo vyombo vya kijamii vinavyohusika na huduma ya maji (CBWSOs) kwa mafunzo na utaalamu wa uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji.

Pia, kuhamasisha wananchi kuhusu usafi wa mazingira, uhifadhi, utunzaji vyanzo vya maji na kushirikiana na wadau mbalimbali katika huduma za maji na usafi wa mazingira vijijini.

RUWASA mkoani Mara inawashukuru viongozi wa serikali na kijamii, pamoja na waandishi wa habari kwa ushirikiano mzuri wanaoipatia katika juhudi za kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi vijijini.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages