NEWS

Saturday, 21 September 2024

TANAPA inavyotoa kipaumbele uboreshaji wa miundombinu ya barabara Hifadhi ya Serengeti



Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Juma Kuji (Katikati) akimuongoza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula (kushoto) katika ukaguzi wa miundombinu ya barabara ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, Jumatano iliyopita.
-------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu

Hifadhi ya Taifa Serengeti ni moja ya maeneo maarufu zaidi kwa vivutio vya utalii barani Afrika kama si duniani, ikipambwa zaidi na makundi ya wanyamapori wahamao aina ya nyumbu. Hifadhi hii ipo kaskazini mwa Tanzania ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 14,763

Miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika hifadhi hii ambayo imekuwa ikishinda tuzo za hifadhi bora Afrika, ni uboreshaji wa miundombinu ya barabara zake kwa ajili ya urahisi na uendelevu wa shughuli za utalii.

Barabara nzuri zinawezesha watalii kufikia maeneo ya vivutio kirahisi na kwa usalama, lakini pia zinasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira - tofauti na barabara mbovu ambazo zinaweza kusababisha mmomonyoko wa udongo, uchafuzi wa vyanzo vya maji na kuhatarisha ikolojia inayotegemewa kwa uhifadhi wa wanyamapori.

Kwa upande mwingine, wanasayansi na wataalamu wa uhifadhi wanaweza kufanya tafiti zao hifadhini kwa urahisi kama barabara zinapitika vizuri na kuwafikisha salama kwenye maeneo wanayolenga.

Hivyo, uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika Hifadhi ya Taifa Serengeti ni muhimu sana ili kusaidia kuimarisha utalii, kuhakikisha usalama wa wageni, kuhifadhi mazingira na kuongeza mapato ya hifadhi.

Katika kuzingatia hayo yote, uboreshaji wa miundombinu ya barabara umeendelea kupewa kipaumbele katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa ujumla.

Viongozi wa Hifadhi ya Serengeti, TANAPA na Wizara ya Maliasili na Utalii wamekuwa wakifanya ziara za mara kwa mara kukagua miundombinu ya barabara katika hifadhi hii ili kujiridhisha na uimara wake.

Mfano, Jumatano iliyopita, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula alianza ziara ya siku tatu ya kukagua miundombinu ya barabara na huduma za utalii ndani ya hifadhi hii.

Naibu Waziri Kitandula alipokewa na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Juma Kuji na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Ziara hiyo ya Kitandula imekuja miezi michache tangu Kamishna Kuji kukagua miundombinu ya barabara katika hifadhi hii na kuiagiza menejimeti kuharakisha marekebisho ya maeneo yaliyoharibiwa na mvua.

Huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya barabara za hifadhi hii, Kuji alisema TANAPA imejipanga kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara zote katika Hifadhi za Taifa nchini, ikiwemo Serengeti inaboreshwa ili kukidhi matamanio ya wageni wanaozitembelea kujionea na kufurahia vivutio vya utalii.


Wakifurahia sehemu ya mandari 
ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
------------------------------------------

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Dkt Richard Matolo alisema TANAPA imekuwa ikitumia teknolojia mbalimbali kutafuta ufumbuzi wa changamoto za barabara zake.


“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitafanya barabara hizi kupitika wakati wote. Imethibitika kuwa tunaweza kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi,” alisema Mhandisi Matolo.

Afisa Uhifadhi Mkuu anayeshughulikia Mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena alisema lengo la shirika hilo ni kuhakikisha kuwa wageni [watalii] wanapofika hifadhini wanaondoka na kumbukumbu nzuri.

“Tumekuwa na mipango ya muda mrefu na mfupi, na yote tutaitekeleza, lengo likiwa ni wageni wetu wafurahie vivutio hivi vya kipekee duniani,” aliongeza Catherine.

Katika kuunga mkono juhudi za TANAPA za kuboresha miundombinu ya barabara za hifadhi, mwezi uliopita Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) lilikabidhi msaada wa magreda mawili na mtambo wa kushindilia udongo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Hifadhi ya Serengeti.

Mkurugenzi Mkazi wa FZS- Tanzania, Dkt Ezekiel Dembe alikabidhi msaada huo kwa Kamishna Kuji katika hafla iliyofanyika Fort Ikoma, magharibi mwa Hifadhi ya Serengeti, mkoani Mara.

FZS ni Shirika la Uhifadhi la Kimataifa lenye makao makuu nchini Ujerumani ambalo limekuwa likisaidia Serikali ya Tanzania katika kuimarisha uhifadhi, huku uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti ukiwa moja ya vipaumbele vya shirika hilo kwa takribani miaka 60 sasa.

TANAPA inaendelea kuwakumbusha waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu za hifadhi, ikiwemo alama za barababrani ili kuepusha madhara yanayoweza kutokeza, hasa kipindi cha mvua.

Taarifa ya maendeleo ya utalii na miundombinu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti baada ya mvua kubwa za el nino, inaonesha kuwa katika Hifadhi za Taifa 21 zilizopo nchini, Hifadhi ya Serengeti ndiyo yenye mtandao mrefu zaidi wa barabara za udongo na changarawe.

Katika mtandao wa kilomita 3,176 za barabara za Hifadhi ya Serengeti, kilomita 2,407 ni za udongo na 769 ni za changarawe. Kutokana na hoja za kiuhifadhi - hakuna barabara za lami wala zege hifadhini.

Lakini pia, Hifadhi ya Taifa Serengeti ina viwanja vidogo vya ndege vipatavyo saba. Viwanja hivyo ni Serengeti, Kogatende, Lobo, Lamai, Grumeti, Kusini na Fort Ikoma.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages