NEWS

Wednesday, 9 October 2024

RC Mtambi atuma ujumbe kwa wadau wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi.
--------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi ameongoza kikao cha wadau wa uchaguzi kuhusiana na maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu, na kuwataka kuhakikisha unafanyika kwa amani na utulivu.

Akizungumza katika kikao hicho mjini Musoma jana, RC Mtambi aliwataka wadau wote kushiriki kusaidia kuhamasisha wananchi kushiriki katika matukio muhimu ya uchaguzi kwa amani na kufuata miongozo inayotolewa na wasimamizi wa uchaguzi.

“Katika uchaguzi huu tunahitaji amani na utulivu, vyama na wagombea wanadi sera zao na kuwashawishi wananchi wawachague, Serikali ya Mkoa tutahakikisha tunaweka mazingira mazuri ya uchaguzi,” alisema.

RC Mtambi alisema uandikishaji wa wapiga kura Utafanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024 na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapate haki ya kupiga na kupigiwa kura kwenye uchaguzi huo.

Aidha, alisema tarehe ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi huo ni Novemba 1 hadi 7, 2024 huku akitaja nafasi zinazogombewa kuwa ni Mwenyekiti wa Mtaa, Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (kundi mchanganyiko) na kundi la wananwake kwa Halmashauri za Miji na Manispaa.

Kwa Halmashauri za Wilaya, alisema nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti wa Kijiji, Wenyeviti wa Vitongoji vilivyomo katika eneo la kijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (kundi mchanganyiko) na kundi la wanawake.

Alisema uteuzi wa wagombea utafanyika Novemba 8 na viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa kuwasilisha ratiba ya mikutano ya kampeni Novemba 14, 2024.

Kaulimbiu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2024 inasema “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi.”
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages