NEWS

Wednesday, 9 October 2024

‘Intruders’ wapungua mgodi wa North Mara, Rais wa Barrick awashukuru viongozi wa kijamii



Rais na CEO wa Barrick, Dkt Mark Bristow akipiga makofi kufurahia kukabidhi Shule ya Msingi mpya Kenyangi iliyojengwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara katika kijiji cha Matongo. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara. (Picha na Mara Online News)
--------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu

Baada ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kupitia magumu na machungu kwa miaka kadhaa kutokana na tatizo la uvamizi ambao umekuwa ukifanywa na makundi ya watu alimaarufu kama ‘intruders,’ mgodi huo sasa umeanza kupata ahueni.

Na kwa mara ya kwanza, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Dkt Mark Bristow ameonesha kuridhishwa na juhudi za pamoja zinazofanywa kukabiliana na tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Dkt Mark, idadi ya ‘intruders’ katika mgodi huo imepungua kutoka 381 Aprili hadi 65 Agosti mwaka huu.

“Tumepata mafanikio makubwa sana katika kukabiliana na wavamizi. Kwa mfano, idadi ya wavamizi ilipungua kutoka 381 Aprili hadi 65 Agosti [mwaka 2024], hivyo tupo kwenye njia sahihi,” Dkt Mark alisema Jumapilili iliyopita.

Alikuwa akizungumza katika hafla ya kukabidhi Shule ya Msingi mpya ya kisasa ya Kenyangi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime; shule ambayo imejengwa na mgodi wa North Mara kijijini Matongo.


Dkt Mark akizungumza katika hafla hiyo.
---------------------------------------

“Napenda kuwapongeza watu mbalimbali akiwemo mbunge, madiwani, wajumbe wa CDC, wenyeviti wa vijiji na wazee wa mila kwa kazi kubwa mliyofanya kuhakikisha vijana wanaovamia mgodi wanaacha uhalifu huo,” alisema Dkt Mark.

Huku watu wakimpigia makofi kufurahia mafanikio hayo, Rais na CEO huyo wa Barrick aliendelea kuitia moyo jamii inayozunguka mgodi wa North Mara na kuiomba kutobali watu wachache kuirudisha nyuma kimaendeleo.

“Hakuna mtu anayeweza kufurahia mtu mwingine avamie na kuvunja nyumba yake, kwa hiyo tusiruhusu wavamizi. Naamini tukifanya kazi kwa pamoja tunaweza kutatua changamoto za kiulinzi katika mgodi huu.

“Sisi ni jamii moja, na mnaona hata leo tunafurahia matunda ya ushirikiano na ujirani mwema. Tuendelee kushirikiana ili tuendelee kuvuna matunda ya mgodi huu,” alisisitiza Dkt Mark.

Aliiomba jamii inayozuguka mgodi huo kuendelea kusaidia kukemea na kupiga vita uvamizi katika mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Watu wengi walionekana kujawa furaha na matumaini kutokana na ujumbe huo muhimu, wakiamini wako kwenye njia sahihi ya kuendeleza mapambano dhidi ya wavamizi wa mgodi huo.

Dkt Mark, Mbunge Mwita Waitara na viongozi wa mgodi wa North Mara wakiwa katika picha ya pamoja na wazee wa mila.
---------------------------------------

Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara alikazia hoja ya ushirikiano katika kukemea na kupiga vita uhalifu huo, ikiwa ni pamoja na kuwakataa watu wanaouchochea kwa maslahi yao binafsi.

“Kuna nguvu kinzani inayoshawishi vijana kwenda kuvamia mgodi kwamba ni mali yao, lakini viongozi lazima tusimamie kwamba kuvamia mgodi ni kosa na ukipatikana utachukuliwa hatua, na huo ndio ukweli,” alisisitiza mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC), Godfrey Kegoye alisema viongozi wa kijamii wamekuwa wakishiriki moka kwa moja kuhamasisha vijana kuacha kuvamia mgodi huo.

“Sisi pia tunafurahia kupungua kwa uvamizi mgodini. Hatupendi kuona mgodi unavamiwa. Tutazidi kuongeza jitihada ili kuhakikisha uvumizi unapungua kama si kuisha kabisa,” alisema Kegoye ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matongo - aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime katika hafla hiyo.

Aidha, Kegoye alimmiminia sifa Dkt Mark akisema ni kiongozi msikivu na ambaye anatekeleza kwa vitenda maendeleo anayoiahidi jamii inayozunguka mgodi huo.

“Tunakushukuru Dkt Mark, ukiahidi unatekeleza kwa vitendo,” alisema Mwenyekiti huyo wa CDC katika mgodi wa North Mara.


Dkt Mark katika picha ya 
pamoja na viongozi mbalimbali.
------------------------------------

Kupungua kwa ‘intruders’ kunatazamwa kama mafanikio makubwa ya mgodi, jamii na wadau wa maendeleo ambao wangependa kuona uwekezaji endelevu katika mgodi huo ambao umetengeneza fursa nyingi za kiuchumi sio tu katika vijiji jirani, bali pia wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla.

Cha kufurahisha zaidi, viongozi wa kijamii kwenye maeneo yanayozunguka mgodi huo wameonesha utayari wa kushirikiana kuhakikisha vitendo vya uvamizi, wizi wa mawe yenye dhahabu na uharibifu wa miundombinu haviendelei mgodini.

“Hii si kazi ya mtu mmoja, bali ni jitihada za pamoja za watu wote kwenye mapambano haya, hatuwezi kuwa na maendeleo bila kuwa na amani,” mmoja wa viongozi wa vijiji aliiambia Mara Online News.

Kwa ujumla kila mmoja anajiona ana jukumu la kusaidia kuimarisha usalama wa mgodi, kuendeleza uhusiano kati ya mgodi huo na jamii inayouzunguka, kwani juhudi za pamoja zinaweza kufanikisha mambo makubwa zaidi.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages