NEWS

Wednesday, 9 October 2024

DC Bunda ataja takwimu za vifo Ziwa Victoria akipokea msaada wa vifaa okozi kutoka LVBC



Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dkt Vicent Naano (kulia) akipokea msaada wa jaketi okozi kutoka kwa Katibu Mtendaji wa LVBC, Dkt Masinde Bwire kwa ajili ya wakazi wa kata ya Igundu. (Na Mpigapicha Wetu)
-----------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Bunda

Watu zaidi ya wawili hufariki dunia katika Ziwa Victoria kila mwezi wilayani Bunda, Mara kutokana na ajali mbalimbali wakati wa safari ama shughuli za kiuchumi.

Takwimu hizo zilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt Vicent Naano wakati akipokea msaada wa vifaa okozi kutoka Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kufuatia ajali ya mtumbwi iliyotokea Septemba 15, 2024 katika kijiji cha Igundu na kusababisha vifo vya watu sita.

Dkt Naano alisema asilimia kubwa ya wakazi wa wilaya hiyo uchumi wao unategemea Ziwa Victoria, hivyo usafiri na shughuli ndani ya ziwa hilo ni jambo la kawaida licha ya ajali za mara kwa mara ambazo pia husababisha vifo vya watu.

"Ajali zinatokea ama wakiwa wanasafiri, au wanafanya shughuli zao na tumekuwa tukipoteza watu wengi, yaani kila mwezi lazima kunatokea vifo na tayari tumebaini kuwa vifo vingine vinatokana na watu kutozingatia sheria za usafiri salama majini," alisema

Kutokana na hali hiyo, Dkt Naano alisema tayari ofisi yake imeanza kampeni maalum ya kuelimisha jamii kuzingatia suala zima la usalama wawapo majini.

Alifafanua kuwa kampeni hiyo mbali na kushirikisha wataalamu kutoka ofisi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), pia inahusiha maofisa kutoka halmashauri mbili za wilaya hiyo kuelimisha wananchi.

"Tuna boti maalum kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato yatokanayo na ziwa hili, lakini pia boti hiyo imeanza kutumika kutoa elimu kwa wananchi, naamini jitihada zote hizi zitasaidia kupunguza ajali zinazotokea ndani ya ziwa letu," alisema kiongozi huyo wa wilaya.

Katibu Mtendaji wa LVBC, Dkt Masinde Bwire alisema ofisi yake imeamua kutoa msaada wa vifaa okozi kufuatia ajali iliyotokea katika kijiji cha Igundu na kusababisha vifo vya watu sita baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kutoka harusini kuzama.

Chanzo cha ajali hiyo ambayo watu 14 walinusurika kilielezwa kuwa ni uzito mkubwa kuliko uwezo wa mtumbwi uliohusika ambapo pia haukuwa maalum kwa ajili ya kusafirisha abiria.


Ofisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Mara, Hezron Lusangija akitoa malekezo namna ya kuvaa jaketi okozi.
--------------------------------

Dkt Bwire alisema ipo haja ya mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kudhibiti ajali ambazo zimekuwa zikitokea ndani ya ziwa hilo na kusababisha vifo ya watu wengi kila mwaka katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Alisema kwa upande wa LVBC tayari wameanza kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya uokozi katika nchi zote tatu huku kituo kikuu kikijengwa mkoani Mwanza, na kwamba vituo hivyo vitakapokamilika vitasaidia kupatikana taarifa kwa haraka za ajali na uokoaji kufanyika mpema, miongoni mwa mambo mengine.

"Hili ziwa halitakiwi kuwa lango la kaburi, halitakiwi kuwa chanzo cha watu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kupoteza maisha, bali linatakiwa kuwa chanzo cha uchumi wa watu wa jumuiya. Hatutaki tuwe tunakuja hapa kila mwaka kwa sababu ya vifo, bali tuwe tunkuja hapa kwa ajili ya miradi mikubwa ya kimaendeleo na kiuchumi," alisema Dkt Bwire.

Alisema matukio ya miaka miwili yaliyotokea katika kata ya Igundu na kusababisha vifo vya watu 20,wakiwemo wanafunzi 13 wa Shule ya Msingi Bulomba, yanasikitisha na kwamba ipo haja ya kuhakikisha matukio kama hayo hayatokeo tena.

Wakizungumza baada ya kupokea msaada wa maboya okozi kutoka Kamisheni hiyo, baadhi ya wakazi wa kijiji cha Igundu walisema ajali nyingi zinazotokea zinasabaishwa na wamiliki wa mitumbwi kutofuata sheria na taratibu.

Nyanjiga Mafuru alisema ili kukomesha ajali hizo hatua kali zichukuliwe dhidi ya watu, hususan wamiliki wa mitumbwi ya uvuvi wanaotumia kusafirisha abiria.

"Unakuta mtumbwi ni kwa ajili ya uvuvi, tena una uwezo wa kubeba watu wanne au watano, lakini unabadilishiwa matumizi na kubeba watu zaidi ya 20, hii ni hatari tunaomba hatua zihukuliwe," alisema Nyamambara Bruno.

Jaketi okozi zaidi ya 20 zilitolewa na Kamisheni hiyo na kukabidhiwa katika kata ya Igundu kwa ajli ya matumizi ya wakazi wake wanapotumia usafiri wa majini.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages