NEWS

Monday, 14 October 2024

Tunamuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuwafikishia wananchi huduma ya maji, hakuna atakayeachwa

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

NA MWANDISHI MAALUMU

--------------------------------------


Katika kuadhimisha Miaka 25 ya Kumbukizi ya Kifo cha Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius K. Nyerere leo Oktoba 14, 2024, ni muhimu pia kuangazia juhudi zinazofanywa na serikali katika uboreshaji wa huduma ya maji kwa wananchi, suala ambalo alilitilia mkazo enzi za uongozi wake.


Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita, Dkt Samia Suluhu Hassan ameendelea kudhihirisha kwa vitendo dhamira yake ya “kumtua mama ndoo ya maji kichwani” ili kuhakikisha Tanzania inapiga hatua kubwa katika suala zima la huduma ya maji ya bomba na kuleta mafanikio katika nyanja mbalimbali.


Kama ambavyo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipigania maendeleo ya Watanzania wote bila ubaguzi kwa lengo la kujenga taifa lenye nguvu na ustawi, ndivyo Rais Samia anavyoendelea kuweka msukumo wa uboreshaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi mijini na vijijini, akizingatia kuwa maji hayana mbadala, na maji ni uhai wa kila kiumbe na mazingira.


Rais Samia ameweka historia kwa ‘kutafuna fupa’ lililokuwa limeshindikana la mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe ambao ulikaa zaidi ya miaka 15 na kubeba sifa ya kutokamilika kwa muda mrefu, lakini sasa unafanya kazi.


Maono ya Rais Samia yanatekelezwa na Wizara ya Maji katika kuwaletea wananchi maendeleo, na hivi sasa kiongozi huyo wa nchi amewezesha kila eneo lililokuwa halijafikiwa kuchimbiwa kisima cha majisafi - kupitia mpango wa kuchimba visima 900 aliouzindua hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma.


Shukrani pia kwa wadau wa maendeleo ambao wanaunga mkono kazi ya kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi mijini na vijijini.


Novemba 2023, Tanzania ilipongezwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt Victoria Kwakwa katika mkutano wa viongozi wa kanda hiyo uliohusu masuala ya upatikanaji wa majisafi na salama na usafi wa mazingira nchini Ethiopia.


Dkt Kwakwa aliipongeza Tanzania kwa kutekeleza kwa ubora na viwango vya juu Programu ya Uendelevu wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (PforR) na kuwa kinara kati ya nchi zaidi ya 50 duniani zinazotekeleza programu hiyo.


Kutokana na maendeleo hayo, Dkt Kwakwa aliiomba Tanzania kueleza uzoefu wa mafanikio yake katika miradi ya maji na huduma kwa wananchi kwa nchi nyingine za Mashariki na Kusini mwa Afrika zilizoshiriki mkutano huo.


Kwa mipango madhubuti inayoendelezwa na serikali, hakuna Mtanzania atakayeachwa katika miradi mbalimbali ya maji - mikubwa na midogo inayoendelea kutekelezwa nchini. 


Waziri wa Maji, Jumaa Aweso anasema kazi mbalimbali zinaendelea katika kila kona ya nchi ili kufikia lengo la upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini. 


Takwimu zinaonesha upatikanaji wa majisafi na salama vijijini umeongezeka kutoka wastani wa asilimia 70.1 mwaka 2021 hadi asilimia 77 Desemba 2023, na kwa upande wa mijini umeongezeka kutoka wastani wa asilimia 84 mwaka 2021 hadi wastani wa asilimia 88 Desemba 2023.


Mageuzi makubwa katika sekta ya maji yanashuhudiwa pia katika mkoa wa Mara ambapo miradi mingi ya majisafi na salama ya bomba imeendelea kutekelezwa mijini na vijijini kutokana na mabilioni ya fedha zinazotengwa na serikali kila mwaka.


Miongoni mwa miradi hiyo ambayo inatekelezwa kupitia MUWASA na RUWASA ni pamoja na ule wa Mugango-Kiabakari-Butiama unatoa maji Ziwa Victoria wenye thamani ya shilingi bilioni 70.5.

 

Mradi mwingine wa maji kutoka Ziwa Victoria ni ule wa Rorya na Tarime unaoendelea kutekelezwa - ambao umetengewa shilingi bilioni 134 kutoka serikalini.


Kinsingi, hadi sasa miradi mingi imekamilika na mingine inaendelea kutekelezwa kwa kasi ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji ya bomba kwa wananchi katika wilaya za Musoma, Bunda, Serengeti, Tarime, Rorya na Butiama zinazounda mkoa huo.


Moja ya kichocheo cha mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta ya maji nchini, ni ushirikishwaji wa jamii katika kufanikisha mahitaji muhimu ya huduma ya maji. 


Mfano mojawapo ni programu ya Mpango wa Matokeo ambao kutokana na ushirikishwaji wa wananchi na uwajibikaji umeleta matokeo bora. Awali, sekta ya maji ilipata Dola milioni 350, na ndani ya miaka mitatu ilikuwa imepeleka maji kwa wanufaika wapya milioni 4.7 maeneo ya vijijini.


Juhudi hizo, Waziri Aweso anasema zimewezesha pia wananchi milioni 6.6 kuwa na vyoo bora vijijini katika mikoa 17, ikiwa ni matokeo makubwa kuliko nchi nyingine duniani zinazotekeleza Mpango wa Matokeo chini ya ufadhili kutoka Benki ya Dunia (WB).


Pamoja na programu hiyo, Wizara ya Maji imejipambanua katika kufanikisha kazi za kufikisha huduma ya maji kwa jamii kwa kutekeleza mambo mbalimbali, kama vile kuongeza kasi ya ukarabati na upanuzi wa miradi ya maji katika miji 28 inayolenga kunufaisha wananchi zaidi ya milioni moja.


Kingine, ni kuongeza kasi ya ujenzi wa bwawa la Farkwa na mtambo wa kusafisha na kutibu maji ili kuondoa kero ya uhaba wa maji katika jiji la Dodoma na miji ya Chamwino, Bahi na Chemba.


Pia, kupeleka maji katika maeneo yenye upungufu, ikiwa ni pamoja na kujenga mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka katika miji ya Singida na Dodoma ili kuondoa kabisa kero ya uhaba wa maji katika jiji la Dodoma ambalo ni makao makuu ya nchi.


Vile vile, kukamilisha ujenzi wa bwawa la Kidunda ambalo litapunguza tatizo la uhaba wa maji katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam ambalo ni chanzo kikubwa cha mapato ya serikali.


Juhudi nyingine ni kuendelea kujenga miradi mikubwa inayotumia vyanzo vya maji vya uhakika, ikiwemo mito mikubwa na maziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa; na kutafiti maji chini ya ardhi kwa ajili ya kuchimba visima virefu na kujenga miundombinu ya kusambaza maji kwa wananchi.


Serikali inafanya juhudi zote hizi kwa kutambua kuwa maji ni rasilimali muhimu kwa maisha ya binadamu - yanayohusisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, lakini pia ni kichocheo cha shughuli za majumbani, kilimo cha umwagiliaji, umeme wa nguvu za maji, viwanda, uvuvi, mifugo, madini na utalii. 


Kwa ujumla, upatikanaji wa maji kwa ajili ya sekta mbalimbali, na usimamizi madhubuti wa rasilimali za maji ni msingi wa shughuli zote za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa usalama wa taifa.


Hivyo basi, katika kuadhimisha siku hii ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, pia tuna kila sababu ya kuipongeza serikali na kujivunia uongozi wa Rais Samia kwa juhudi kubwa anazofanya kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi mijini na vijijini.


Kwa kuzingatia ukweli kuwa maji ni uhai, ni muhimu kwa kila mwananchi kutambua kwamba ana jukumu la kulinda, kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji na miundombinu yake. 


Tunaposhirikiana katika kulinda, kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji, tunaweza kufikia malengo ya maendeleo endelevu, na kuendelea kuijenga Tanzania iliyo bora kwa ustawi wa maisha ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages