NA GODFREY MARWA, Tarime
-----------------------------------------
Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Right to Play wameendelea na kampeni ya kuhamasisha jamii kumpatia mtoto wa kike elimu.
Msisitizo huo ulitolewa Ijumaa iliyopita wakati wa tamasha la michezo na burudani lililoandaliwa na taasisi hizo katika Shule ya Msingi Nyankoni iliyopo kata ya Itiryo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).
Afisa Mradi kutoka AICT, Daniel Fungo alisisitiza kuwa elimu ni haki ya kila mtoto, hivyo jamii ina wajibu wa kumpeleka shule na kumlinda mtoto wa kike dhidi ya vitendo vya ukatili ukiwemo ukeketaji.
"Kila mtoto ana haki ya kupata elimu, taarifa zitolewe kwa wale wanaowanyima watoto kupata elimu, lengo letu ni kuhamasisha suala la elimu kwa mtoto wa kike," alisema Fungo.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Itiryo, Pendo Mushi alizishukuru taasisi hizo na kusema serikali ipo tayari kushirikiana nazo katika kukomesha vitendo ya ukatili wa kijinsia katika jamii.
"Tamasha ni zuri sana, watoto wanajifunza mambo mbalimbali kupitia michezo. Mtoto wa kike mzazi akikuachisha shule kwa ajili ya ukeketaji toa taarifa - pamoja na matendo ya ukatili na changamoto ili usaidiwe na serikali kwa maendeleo endelevu.
“Mtoto wa kike akisomeshwa anaweza kuwa yeyote, usikubali kwenda kulima na kuacha masomo," alisema Pendo.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyankoni, Paulo Desdery Akonay aliishauri jamii kuwekeza kwa kusomesha watoto wote bila kujali jinsia wala hali yao kwani serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira rafiki na wezeshi kuhakikisha kila mtoto nchini anapata elimu bila malipo kuanzia shule za awali na msingi hadi sekondari ya juu.
No comments:
Post a Comment