NEWS

Friday, 1 November 2024

Profesa Kithure Kindiki aapishwa kuwa Naibu Rais mpya wa Kenya, amshukuru Rais Ruto, amuahidi utiifu



Prof Kithure Kindiki akila kiapo

Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Kenya, Prof Kithure Kindiki ameapishwa rasmi kuwa Naibu Rais mpya wa Kenya katika hafla iliyofanyika jijini Nairobi leo Novemba 1, 2024.

Kithure Kindiki anachukua nafasi ya Rigathi Gachagua aliyeondolewa madarakani.

Anachukuwa wadhfa huo baada ya siku kadhaa za makabiliano ya mahakamani kati ya mawakili wa Gachagua na wale wa Serikali.

Awali, Mkuu wa Utumishi wa Umma nchini Kenya, Felix Kosgei alitangaza kwenye gazeti la Serikali kamati ya wanachama 23 kusimamia kuandaliwa kwa hafla ya kuapishwa kwa Naibu Rais Mteule Kithure Kindiki.

Wakati huo huo, Serikali imetangaza Ijumaa Novemba 1, 2024 kuwa Sikukuu ya Kitaifa.

Hayo yanajiri muda mfupi baada ya Mahakama Kuu nchini Kenya kuondoa amri zinazomzuia Naibu Rais Mteule Kithure Kindiki kuapishwa.

Kithure Kindiki ni nani?
Kithure Kindiki alizaliwa Julai 16, 1972 katika kijiji cha Irunduni, eneo bunge la Tharaka, katikati mwa Kenya.

Ni wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya mwenye tajriba ya miaka 21. Prof Kindiki ndiye Waziri pekee wa Baraza la Mawaziri aliyehifadhi nafasi yake tangu alipoteuliwa Septemba 2022.

Kindiki ana Shahada ya Kwanza ya Sheria (LLB) kutoka Chuo Kikuu cha Moi, Diploma ya Uzamili ya Sheria kutoka Shule ya Sheria ya Kenya, Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M), na Shahada ya Uzamivu (Ph.D.) katika Sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini.

Rafiki zake wamemtaja kuwa mtumishi wa umma na Profesa wa Sheria mwenye rekodi nzuri na uzoefu mkubwa katika utawala, sera za umma, utungaji wa sheria, ushauri wa kisheria na masuala ya katiba katika ngazi ya manispaa na kimataifa.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani ana uhusiano wa muda mrefu na Rais William Ruto na alikuwa wakili wake alipokuwa akikabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).


Prof Kindiki na Rais Ruto
----------------------------------

Kindiki alikuwa mstari wa mbele miongoni mwa waliokuwa wakizingatiwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto katika uchaguzi wa mwaka wa 2022 lakini baadaye nafasi hiyo akapewa Rigathi Gachagua ambaye alitimuliwa ofisini kupitia kura ya maseneta.

Kabla ya kujiunga na siasa, Kindiki alifundisha sheria na kushikilia nyadhifa mbalimbali za utawala katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Moi na Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alianza taaluma yake kama Mhadhiri Msaidizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Moi mara baada ya kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Sheria.

Kisha alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kama Mhadhiri baada ya kuhitimu na Shahada ya Uzamivu katika Sheria ya Kimataifa ambapo alipanda cheo hadi Mkuu wa Idara ya Sheria ya Umma akiwa na umri wa miaka 33.

Baadaye alihudumu kama Mhadhiri Mshirika akiwa na umri wa miaka 35.

Kisha Kindiki alipandishwa cheo hadi wadhifa wa Profesa Mshiriki wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Ameandika machapisho 35, yakiwemo vitabu na makala katika majarida ya ndani na kimataifa kuhusu Sheria na Utungaji Sera.

Kindiki ni mjumbe wa Baraza la Kitaaluma la Mfumo wa Umoja wa Mataifa (ACUNS), Jumuiya ya Kimataifa ya Utafiti wa Uhamiaji wa Kulazimishwa (IASFM), Tume ya Kimataifa ya Wanasheria (ICJ), Jumuiya ya Wanasheria ya Afrika Mashariki (EALS) na Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK).



Kabla ya kuteuliwa katika Baraza la Mawaziri, Kindiki alihudumu kama Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi, kuanzia mwaka 2013 hadi 2022.

Kati ya mwaka 2013 na 2017, alihudumu kama Kiongozi wa Wengi katika Seneti na kutoka mwaka 2017, alipanda cheo na kuwa Naibu Spika wa Seneti.

Katika nafasi yake kama Kiongozi wa Wengi katika Seneti, aliongoza ajenda ya kutunga Sheria ya Chama cha Wengi katika Seneti na aliwahi kuwa kiongozi wa Walio Wengi.

Akiwa Naibu Spika wa Seneti, Kindiki alimsaidia Spika wa Seneti katika kusimamia vikao na mijadala katika Bunge la Seneti na kutekeleza kanuni za utaratibu na michakato ya bunge.

Pia, aliendesha majukumu ya uangalizi katika usimamizi wa kaunti na kushiriki katika kutunga sheria kuhusu masuala yanayohusu kaunti.

Katika kipindi cha miaka miwili aliyohudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kindiki ameongoza na kusimamia mafanikio ya hatua kubwa na mageuzi mbalimbali katika wizara hiyo, ikiwa ni pamoja na Uboreshaji wa Vifaa vya Polisi, kukamilisha mkakati wa kuanza utekelezaji wa Maboresho ya Jeshi la Polisi, na kuboresha taratibu za awali za uhakiki wa utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.

Kindiki pia amesimamia utambuzi wa vikundi vya wachache na jamii zisizo na utaifa kwa kuhakikisha wanapokea uraia wa Kenya, kutekeleza Sheria ya Mashirika ya Manufaa ya Umma, kuimarisha vita dhidi ya ujambazi na ukosefu wa usalama kote nchini, kuandaa pendekezo la kisheria la kurekebisha Serikali ya Kitaifa, na Sheria ya Uratibu ya mwaka 2013 kuwatambua rasmi wazee wa vijiji katika kila kitengo.

Aidha, Kindiki ameongoza uandikishaji wa wafungwa 13,120 katika programu za elimu rasmi, miongoni mwa zingine.

Amshukuru Rais Ruto
Akizungumza baada ya kuapishwa, Naibu Rais mpya wa Kenya Kithure Kindiki amemshkuru rais William Ruto kwa kumteua kuwa naibu wake.

Akihutubia umati mkubwa wa watu muda mfupi baada ya kuapishwa, Kindiki ameahidi kuwa mtiifu kwa Rais Willima Ruto.

Aidha, Prof Kindiki amewashukuru wale wote waliochangia mafanikio yake.

''Ninakuahidi Mheshimiwa Rais kuwa nitahudumu chini yako na kukuunga mkono kuiongoza nchi hii,'' amesema na kuongeza''Naomba Mungu anisaidie kutekeleza majukumu haya.''

Chanzo: BBC
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages