Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ngw'ilabazu Ludigija (katikati waliokaa) katika picha ya pamoja na baadhi wa watoa huduma kwenye semina ya wastaafu watarajiwa inayofanyika Mwanza leo.
-------------------------------------------
Mfuko wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (PSSSF) umelipa shilingi zaidi trillion 10.46 kwa wanufaika 310,456 tangu kuanzishwa kwake miaka sita iliyopita.
Malipo hayo ni pamoja na mafao ya uzeeni, ulemavu, kifo, wategemezi, kukosa ajira, ugonjwa na uzazi.
Hayo yamebainishwa leo katika semina kwa wastaafu watarajiwa inayofanyika jijini Mwanza, ikiwa ni mkakati wa mfuko huo kuwaandaa wastaafu watarajiwa kukabiliana na maisha nje ya mfumo rasmi wa ajira katika maisha ya uzeeni.
Akitoa takwimu hizo, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo amesema mbali ya mafao kwa wanufaika, ndani ya mwaka huu wa fedha 2024/2025, Mfuko unatarajia kulipa mafao ya uzeeni kwa wastaafu 11,622, ambapo shilingi bilioni 560.8 zitatumika sambamba na shilingi bilioni 980.3 kwa wanufaika takriban 190,000 wa mafao ya jumla.
"Kutokana na ukubwa wa mafao yanayolipwa, shirika linaona kuna haja kubwa ya kuwaandaa wastaafu watarajiwa juu ya namna bora ya kupangilia maisha yao na kutumia vizuri mafao yao," amesema Magambo.
Ameongeza kuwa mkakati wa semina hizo zinazofanyika kila mwaka unalenga kuwanufaisha wanachama wa PSSSF waliobakiza kipindi kisichozidi miaka miwili kabla ya kustaafu.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ngw'ilabazu Ludigija, mbali na kulipongeza shirika kwa kuandaa semina hizo, amewataka wastaafu watarajiwa kuzingatia kwa makini mafunzo wanayopewa ili mafao yao yalete tija iliyokudiwa.
Ludigija ametoa changamoto kwa watumishi wa PSSSF kuzingatia weledi na kufanya kazi kwa uadilifu ili kuhakikisha wanachama wake waliolitumikia Taifa kwa miaka mingi wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria.
"Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa PSSSF inatimiza majukumu yake vema na kuusimamia Mfuko huu kwa karibu sana kuhakikisha michango ya wanachama iko salama muda wote,” amesema.
Nao wastaafu watarajiwa Rose Mhina na Saida Batenga wamesema semina hiyo itawasaidia wanapojipanga kustaafu mapema mwakani.
Mhina amesema hata kabla ya kupokea mafao yake, tayari amejipanga kwa kuanzisha vitega uchumi kadhaa.
Mada kadhaa zitatolewa na wataalamu mbalimbali wakiwemo wa afya ya akili wenye jukumu la kuwaandaa wastaafu watarajiwa kisaikolojia na maisha yajayo, hasa matumizi salama ya mafao yao.
No comments:
Post a Comment