Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Christopher Mwita Gachuma (kushoto) na wazee wa mila waliomsimika kuwa Chifu wa Koo ya Wakenye wilayani Tarime. (Picha na Godfrey Marwa)
-------------------------------------------
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Christopher Mwita Gachuma amesimikwa kuwa Chifu wa Koo ya Wakenye katika kabila la Wakurya wilayani Tarime, Mara.
Hafla ya kumsimika ilifanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Manga Novemba 9, 2024, ambapo wazee wa mila wa koo ya Wakenya walisema wamempa uchifu kuonesha kutambua na kuthamini mchango wake mkubwa katika maendeleo ya jamii hiyo.
Akizungumza baada ya kusimikwa, Gachuma aliahidi kuanzisha ujenzi wa shule ya sekondari ya juu (high school) ya wavulana katika eneo la Komaswa ili kuchochea maendeleo ya koo hiyo.
MNEC Christopher Mwita Gachuma akiwa
na vifaa vya Uchifu baada ya kusimikwa.
----------------------------------------
----------------------------------------
“Bukenye tujenge sekondari nyingine ya high school ya wavula, tulete maendeleo kwa pamoja, tutapambana tufikishe sehemu ambayo serikali inaweza ikaja, maana haiji kwa mtu aliyelala," alisema.
Wakati huo huo, Bodi ya Shule ya Sekondari Manga imemtunuku Gachuma cheti maalum kutambua mchango wake wa hali na mali katika kufanikisha ujenzi wa shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha sita.
Mgeni rasmi karika hafla hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa alimpongeza Chifu Gachuma akimtaja kama mtu wa kimataifa kutokana na mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya jamii.
“Hongera Gachuma, wewe ni mtu wa kimataifa. Kwenu ni kwenu, leo umeheshimishwa na wazee wa mila kuwa kiongozi wao mkubwa, hii ni nafasi kubwa. CCM inatambua uchifu na Mwalimu [Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere] alikuwa anatambua machifu," alisema Chandi.
Naye Chifu wa Koo ya Wasimbiti, Alfred Nyihita alimpongeza Gachuma huku akimtaja kama shujaa wa maendeleo. “Gachuma ni mpenda maendeleo,” alisema.
Hafla ya kumsimika Gachuma kuwa Chifu wa Wakenye ilihudhuriwa pia na mfanyabiashara maarufu Peter Zakaria, viongozi wa dini na serikali, miongoni mwa wengine.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>PSSSF yalipa trilioni 10.46 kwa wanufaika zaidi ya 300,000 tangu ianzishwe miaka 6 iliyopita
>>Askari Uhifadhi auawa na tembo Tarime Vijijini
>>Mkurugenzi wa Kampuni ya Matari's Sales and Investment aipa Sekondari ya Bungurere msaada wa photocopy, kompyuta
>>NECTA yatangaza matokeo ya darasa la saba 2024
No comments:
Post a Comment