NEWS

Sunday, 29 December 2024

Bunda: Dkt Mukama anavyoibeba Mwibara kuchochea maendeleo ya wananchi



Dkt Wilson Mukama

NA MWANDISHI MAALUMU

WANANCHI wa tarafa za Kenkombyo na Nansimo zilizopo jimbo la Mwibata katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara wana kila sababu ya kujivunia mdau wa maendeleo Dkt Wilson Mukama, ambaye ameonesha moyo wa kujitolea kuchangia maendeleo yao kupitia miradi ya kijamii na kiuchumi.

Dkt Mukama anafanya hivyo kuunga juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya wananchi.

Amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu katika jimbo la Mwibara. Shule za msingi na sekondari zimenufaika na misaada yake mbalimbali, ikiwemo ya vifaa vya kisasa vya kujifunzia.

Katika kipindi cha takriban miezi miwili, Dkt Mukama ameweza kugharimia ukarabati wa vyumba vinne vya madarasa na ofisi moja ya walimu katika Shule ya Msingi Igunda A.

Sehemu ya majengo manne na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Igunda A yaliyokarabatiwa kwa gharama zilizotolewa na Dkt Wilson Mukama.
--------------------------------------

Kwa upande wa Shule ya Msingi Isanju amechangia shilingi milioni moja kwa ajili ya kujenga vyoo, kununua ‘photocopy machine’ na kompyuta. Hali kadhalika, Dkt Mukama ameipatia Shule ya Msingi Mwiruruma msaada wa ‘photocopy machine’ mpya na kompyuta.

“Kwenye Shule ya Msingi Nafuba nimechangia ujenzi wa barabara na saruji mifuko 200,” Dkt Mukama alisema katika mazungumzo na Sauti ya Mara wilayani Bunda jana.

Kwa upande mwingine, ameipa Shule ya Sekondari Kwiramba msaada wa shilingi milioni 1.5 taslimu na ahadi ya shilingi milioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi, ununuzi wa kompyuta sita, miche 200 ya miembe inayokomaa kwa muda mfupi, saruji mifuko 80, matenki mawili ya maji na jezi za michezo.

Vilevile, ameipatia Shue ya Sekondari Sunsi msaada wa shilingi milioni moja, ‘photocopy machine’ na kompyuta nne, huku Shule ya Sekondari Chisorya akiichangia shilingi milioni moja, saruji mifuko 100, matenki mawili ya maji na kompyuta nne.

Kwenye ujenzi wa Shule ya Sekondari Makwa, amejitolea kununua mashine ya kusukuma maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya kutumika katika ujenzi huo.


Dkt Wilson Mukama (kulia) akikabidhi msaada wa ‘photocopy machine’ mpya na kompyuta katika Shule ya Msingi Mwiruruma iliyopo kata Iramba.
-------------------------------------

“Aidha, katika uchaguzi uliopita wa viongozi wa Serikali za Mitaa, nilishiriki kikamilifu katika kukisaidia chama chetu [CCM] kikapata ushindi wa kishindo,” anasema Dkt Mukama.

Zaidi ya hayo, Dkt Mukama ameahidi kuijenga upya ofisi ya CCM Kata ya Kibara kwa gharama inayokadiriwa kuwa shilingi zaidi ya milioni 130. Pia, ameahidi kukipatia kikundi cha waendesha pikipiki za abiria [bodaboda] kata ya Kibara msaada wa viti 40.

Sehemu ya jengo la CCM Kata ya Kibara ambalo Dkt Wilson Mukama amekarabati, lina ofisi 10, fremu 13 za biashara na ukumbi mkubwa wa mikutano.
----------------------------------

Aidha, Dkt Mukama amekuwa akiwawasaidia wananchi wakati wa matatizo na mahitaji mbalimbali kama vile matibabu na misiba.

Lakini pia, ana mpango wa kuunda vikundi 12 kutoka kata zote za jimbo la Mwibara kwa ajili ya mradi wa upandaji miti ya miembe kama zao la biashara.

Mpango wake mwingine ni kuajiri walimu wenye vigezo katika tarafa za Kenkombyo na Nansimo na kuwalipa posho kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kufundishaji na kuinua taaluma na ufaulu wa wanafunzi katika mitihani.


Mashindano ya Samia Cup Jimbo la Mwibara yalidhaminiwa na Dkt Wilson Mukama.
----------------------------------

Kwa upande wa kilimo, Dkt Mukama ana mpango wa kuwatumia wataalamu kufanya tafiti ili kujua aina ya mazao yanayoweza kustawi kutokana na virutubisha vilivyopo. “Lengo ni kupata mazao mbadala ya kilimo kwa ajili ya biashara,” anasema Dkt Mukama.

Dkt Mukama pia anatazamia kuanzisha kilimo cha mazao ya alizeti, pilipili, vitunguu, karoti na mpunga unaokomaa kwa muda mfupi.

Sambamba na hayo, anafikiria mradi wa kuchimba mabwawa na kupandikiza vifaranga wa Samaki ili kuimarisha uvuvi, miongoni mwa shughuli nyingine za kiuchumi kwa ajili ya wananchi kujipatia kipato.

Pia, katika kulifanya jimbo la Mwibara kuwa sehemu bora kwa ajili ya watu kufanyia shughuli zao, Dkt Mukama ana maono ya kutengeneza fursa zaidi ili kuvutia uwekezaji akiamini kwamba shughuli nyingi za kiuchumi zitaharakisha maendeleo ya wananchi wa Mwibara.


Kimojawapo cha visima vya kuhifadhi maji kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Makwa katani Nampindi, vilivyojengwa chini ya ufadhili wa Dkt Wilson Mukama.
------------------------------------

Kwa hakika, miradi yote hiyo ni nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kisekta na kuboresha maisha ya jamii, shukrani kwa Dkt Mukama kwa maono ya ustawi wa wana-Mwibara.

“Sitasahau pia kutambua michango ya wataalamu na watumishi mbalimbali waliopo katika maeneo yetu, kuwatia moyo kupitia kwa kuwapa motisha ili kuwajengea ari na nguvu ya kutekeleza majukumu yao kwa maendeleo ya jamii.

“Mjadala mkuu wa Mwibara ni maendeleo yenye kasi kwani tumechelewa. Wenye maono kama haya, au zaidi waunganishe nguvu na maono yao ili kuiendeleza Mwibara yetu,” anahitimisha Dkt Mukama.Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages