
Simba
Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News
Serikali imeombwa kuiondolea kata ya Nagusi wilayani Serengeti, Mara tatizo la simba wanaovamia na kuua mifugo ya wanavijiji usiku na mchana.
“Simba wamekuwa tatizo kubwa hapa katani, wanakamata na kuua mifugo ya watu,” Diwani wa Kata ya Nagusi, Andrea Mapinduzi aliiambia Mara Online News kwa simu juzi.
Mfano, Mapindusi alisema kwamba katikati ya Desemba mwaka huu, ng’ombe sita - mali ya Machege Mosi waliuawa na simba saa tatu usiku katika kijiji cha Singisi.
“Pia, Desemba 24, mwaka huu simba walikamata kondoo wawili katani hapa saa saba mchana,” aliongeza diwani huyo kutoka chama tawala - CCM.
Simba hao pia wamekuwa tishio la usalama wa maisha ya wananchi katika kata hiyo inayopakana na maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori.
“Maofisa wa idara ya wanyamapori katika Halmashauri ya Wlaya ya Serengeti wamekuwa wakija kuwatega simba lakini hawajafanikiwa kuwanasa ili kuwarudisha hifadhini,” alisema Diwani Mapinduzi.
Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo pia kuwataka wananchi katani Nagusi kuchukua tahadhari dhidi ya simba hao, ikiwa ni pamoja na kutowatuma watoto kwenda kuchunga mifugo.
“Pia, wananchi waimarishe mazizi ya mifugo kutoka yaliyojengwa kwa miti kwenda ya waya, sambamba na kuanzisha doria za pamoja ili kukabiliana na tatizo hili,” alisema Mapinduzi.
Mara Online News inaendelea na juhudi za kuumpata uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ili kujua hatua zinazochukuliwa kukabili tatizo hilo.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Musoma Vijijini: Sekondari 6 mpya kuanza kupokea kidato cha kwanza Januari 2025
>> Mara: Wanasiasa wapigana vikumbo kujipendekeza kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
>>Korea Kusini:Zaidi ya watu 170 wafariki dunia katika ajali ya ndege
>>Maswi akerwa chuki za kisiasa kukwamisha maendeleo ya wananchi Tarime Vijijini
No comments:
Post a Comment