
Na MwandishI Maalumu/ Mara Online News
Katika hali inayotazamwa kama kujipendekeza kwa wananchi, baadhi ya wanasiasa wamejitokeza kutumia Sikukuu ya Krismasi mwaka huu ‘kujiweka karibu na wananchi’ wa mkoani Mara kuelekea Uchaguzi Mkuu mwakani.
Wanasiasa hao ambao wanaonesha dalili za kuwania ubunge katika majimbo ya mkoa huo, wamejitolea kuwapa wanachama wa vyama vyao na hata wananchi wa kawaida misaada ya fedha kwa ajili ya mahitaji ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Uchunguzi uliofanywa na Mara Online News umebaini kuwa wanasiasa hao wanatumia njia hiyo kama sehemu ya kujenga uhusiano mzuri na wananchi (wapigakura).
“Misaada hii ya fedha ni sehemu ya mikakati ya wanasiasa kujipatia umaarufu kwa wapigakura kuelekea uchaguzi mkuu ujao,” alisema mmoja wa makada maarufu wa kisiasa mkoani Mara.
Wachambuzi wa masuala ya siasa na uongozi wanasema michango ya fedha kwa makundi ya wananchi ni mbinu maarufu inayotumika kuwapata wapigakura, na inatarajiwa kuongezeka kadri uchaguzi mkuu unavyokaribia.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 huenda utakuwa na ushindani mkali kuwahi kutokea, kutokana na dalili zinazooneshwa na wanasiasa za kujiandaa kwa hali na mali ili kuvutia kura za wananchi katika majimbo ya mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment