NEWS

Friday, 13 December 2024

Lissu atangaza ‘vita’ ya kubadilisha uongozi wa juu CHADEMA



Tundu Lissu

Na Mwandishi Wetu

Makamu Mwenyekiti wa chama cha upinzani - CHADEMA Taifa, Tundu Lissu amesema ameshawishika kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho ili kudumisha utamaduni wa kubadilisha viongozi.

Lissu amesema tangu Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2015, kumekuwa na maoni mengi kutoka kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa CHADEMA kumshawishi agombee nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho ili kuingiza damu changa katika uongozi.

“Mara zote nimechukulia ushawishi huo kuwa ulikuwa na nia njema ya kuhakikisha tunaendeleza na kuimarisha utamaduni wa kubadilisha uongozi na madaraka ya uongozi ndani ya chama chetu uliowekwa na viongozi wakuu waanzilishi, yaani Mzee Edwin Mtei na hayati Bob Makani,” alisema Lissu jana wakati akiwahutubia mamia ya wanachama wa CHADEMA jijini Dar es Salaam.

Alisema akina Mtei na hayati Makani walikuwa ni viongozi wenye weledi waliopata elimu wakati wa mkoloni na kupikwa vilivyo katika kuelewa ubaya wa dhana ya kung’ang’ania madaraka.

Kwa sababu ya ufahamu wao wa historia ya madhara kukumbatia madaraka kwa muda mrefu, mzee Mtei na hayati Makani hawakutaka kupata aibu ya kung’olewa madarakani kwa nguvu ya wanachama.

Akiwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Mtei alianzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kuruhusu damu changa ya viongozi vijana kuingia kwenye Kamati Kuu ya CHADEMA.

“Ni muhimu kusisitiza kwamba mabadiliko yote ya uongozi wa juu wa chama yanafanyika kwa njia ya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya chama,” alisema Lissu.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages