NEWS

Thursday, 12 December 2024

Nyambari Nyangwine kuhudhuria uzinduzi wa filamu ya vivutio vya utalii nchini India kesho



Nyambari Nyangwine (katikati) na wasaidizi wake wakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam tayari kwa safari ya kwenda nchini India jana.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Mfanyabiashara wa Tanzania, Nyambari Nyangwine jana aliondoka kwenda nchini India kuhudhuria uzinduzi wa filamu inayoonesha utajiri wa vivuto vya utalii vilivyopo hapa Tanzania.

Uzinduzi huo utafanyika katika jiji la Mumbai, India kesho Desemba 13, 2024.

“Uzinduzi huu wa filamu ya kipekee ambayo inaonesha vivutio vya utalii vilivyopo katika taifa letu la Tanzania, umeandaliwa na Kampuni ya Swahili Safari ya India. Nami nimefurahi kupata mwaliko wa kushiriki,” Nyambari ambaye pia ni mwandishi na mchapishaji maarufu wa vitabu nchini Tanzania aliliambia gazeti hili muda mfupi kabla ya kuanza safari ya kuelekea India.

Inaelezwa kuwa uzinduzi wa filamu hiyo utahudhuriwa na kampuni maarufu za utalii za nchini India na viongozi waandamizi kutoka Tanzania, miongoni mwa mataifa mengine.

“Pia, nitashiriki jukwaa (round table) kuhusu mazingira ya kibiashara ya utalii nchini India Desemba 14, 2024,” aliongeza Nyambari ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime kupitia chama tawala - CCM.

Aidha, Nyambari alisema katika ziara hiyo ya siku tano, pia atatembelea viwanda vya uchapaji vilivyopo katika jiji la Mumbai, India. “Pia, nitatembelea viwanda vya kuchapa madaftari, zikiwemo ‘counter books’ katika mji wa Gujarat,” aliongeza.

Wiki iliyopita, mfanyabiashara huyo wa Tanzania alitanua uwekezaji wake kwa kufungua ofisi katika jiji la Kampala nchini Uganda.

Nyamabari pia hivi karibuni, alianzisha taasisi inayojulikana kwa jina la Nyambari Nyangwine Foundation (NNF) kuunga juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kukuza ajira kwa vijana kupitia ujasiriamali na sekta nyingine kama vile elimu na afya.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages