
Waziri Dkt Dorothy Gwajima (Katikati) akifurahia kuimba na kucheza pamoja na wadau mbalimbali wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyofanyika kitaifa Nyamongo, Tarime jana. (Picha na Mara Online News)
---------------------------------
Mkoa wa Mara siyo kinara tena wa vitendo vya ukatilii wa kijinsia nchini, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt Dorothy Gwajima amesema.
Waziri Gwajima alisema hayo jana wakati wa maadhimisho ya kilele cha kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatilii wa Kijinsia yaliyofanyika kitaifa jana katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe, kilomita chache kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, wilayani Tarime.
“Kati ya mikoa inayoongoza kwa matukio ya ukatili nchini, mkoa wa Mara siyo wa kwanza wala wa pili,” alisema.
Mfano, kwa upande wa ukeketaji, Waziri huyo alisema kwa sasa mikoa ya Arusha na Manyara inaongoza kwa asilimia 43 kila mmoja, huku mkoa wa Mara ukifuata kwa asilimia 28.
Alisifu juhudi za pamoja zinazofanywa na wadau wote wakiwemo viongozi wa Serikali na Jeshi la Polisi mkoani Mara, miongoni mwa wengine kupinga vitendo vya ukatilii wa kijinsia.
“Tunafanya kazi nzuri sana, tuiambie dunia ijue kuwa Mara imeshusha takwimu za ukatili. Na kama imewezekana kwa Mara na mikoa mingine inawezekana,” alisema Waziri Gwajima huku akionekana mwenye furaha kufuatia mkoa huo kupiga hatua kubwa katika kupiga vita vitendo vya ukatilii wa kijinsia.
Aidha, Waziri Gwajima aliwapongeza wadau wote waliosaidia kufanikisha maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatilii wa Kijinsia kufanyika kitaifa mkoani Mara mwaka huu, ambapo Jeshi la Polisi na wadau wengine wakiwemo wanasheria wa kujitegemea kutoka Bowmans waliweza kufikisha elimu ya ukatilii wa kijinsia kwa mamia ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, na wananchi wa kawaida.
Katika maadhimisho hayo, takriban maafisa 250 wa Jeshi la Polisi wanaohusika na dawati la jinsia na ulinzi wa mtoto kutoka maeneo mbalimbali nchini walifika mkoani Mara kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatilii wa kijinsia, hatua ambayo inaelezwa kuleta matokeo chanya baada ya kufikia maelfu ya wananchi.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko alisema mgodi huo una programu mbalimbali za kusaidia kuzuia ukatili wa kijinsia na kukuza usawa wa kijinsia.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara alitaka elimu dhidi ya ukeketaji iendelee kutolewa kwa wananchi wa kawaida wanaoishi vijijini.
“Nimefurahi kuwa ukatili umepungua. Kwa sababu hii ni mila, elimu shirikishi lazima iendelee. Niupongeze Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na wananchi, twendelee kusaidiana kusambaza elimu hii,” alisema Mbunge Waitara kutoka chama tawala - CCM, na ambaye amewahi kuhudumu kama Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita katika wizara mbalimabli.
Katika hatua nyingine, Waziri Gwajima alikabidhi majiko 222 ya gesi kwa baadhi ya wanawake kutoka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara.
Majiko hayo yalitolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa Gas katika kuunga mkono jitihada za serikali za kumtua mama kuni kichwani na kumuepushia adha ya matumizi ya nishati ya kupikia isiyo salama.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kwa Kampuni ya Twiga Minerals.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Mgodi wa North Mara wawapa wanawake msaada wa majiko 222 ya gesi
>>Mjumbe Baraza Kuu UVCCM Taifa Paul Mwikwabe aanza ziara Mara, akabidhi vizibao kwa bodaboda Musoma Vijijini
>>Coastal Union waachana na kipa wao Ley Matampi
>>HABARI PICHA:Waandishi wa habari Mara kushiriki kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
No comments:
Post a Comment