
Maximillian Benjamin akisimamia ujenzi wa barabara ya kwanza ikijengwa kwa nguvu za wananchi hivi karibuni katika kisiwa cha Nafuba wilayani Bunda, Mara.
-------------------------------------
Wananchi wa kijiji cha kisiwa kidogo cha Nafuba kilichopo Ziwa Victoria, wilaya ya Bunda mkoani Mara, wamejitolea kutengeneza barabara yao ya kwanza, hatua ambayo imewaletea mabadiliko makubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa miaka mingi, wananchi hawa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara, hali ambayo ilikuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
Ukosefu wa barabara wala njia ya kupitika hata kwa baiskeli, uliwalazimu wananchi katika kisiwa hiki kusafirisha wagonjwa wao kwa miguu wakiwa wamewabeba kwenye viti, hali ambayo ilisababisha baadhi yao kupoteza maisha kutokana na kuchelewa kufikia vituo vya matibabu.
Lakini hatimaye kwa sasa tabasamu na vicheko vimetawala kwa wananchi hawa, baada umoja na ushirikiano wao kufanikisha ujenzi wa barabara yao ya kwanza kwa kiwango cha mawe na molamu - yenye urefu wa kilomita 5.6.
“Ushiriki wa wananchi ulikuwa kusomba mawe na kifusi cha molamu kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii,” anasema Edward Justas Namwatta, Diwani wa Kata ya Nansimo kilipo kisiwa cha Nakuba.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, wananchi wa Nafuba waliungwa mkono na wadau mbalimbali katika ujenzi wa barabara hii kwa misaada ya vifaa tofauti kama vile saruji, nondo, sururu, koleo, nyaya, unga wa mahindi na sukari ya kuungia uji kwa ajili ya watu waliokuwa kazini.
Anasema wadau hao wa maendeleo, wakiwemo Dkt Wilson Mukama na Mwibara Development Initiative (MDI) pia walitoa msaada wa shilingi zaidi ya milioni tatu kuchangia gharama za ujenzi wa barabara hii.
Aidha, Dkt Mukama pia ametoa msaada wa saruji mifuko 200 kuchangia ujenzi wa shule ya msingi shikizi katika kitongoji cha Kilongo.
“Uwepo wa barabara hii umesaidia kuviunganisha vitongoji vyote vitatu katika kisiwa hiki maana mwanzoni hata baiskeli hazikuweza kupita,” Diwani Namwatta aliiambia Mara Online News wa njia ya simu jana.
Anaendelea: “Kabla ya barabara hii hapakuwa na usafiri kabisa ndani ya kisiwa hiki, lakini kwa sasa kuna usafri wa bodaboda [pikipiki za abiria]. Lakini pia, imesaidia wananchi kufikia huduma za afya na elimu kirahisi.”
“Kukosekana kwa barabara kulisababisha baadhi ya wagonjwa kufa wakisafirishwa kwa miguu kwenda hospitalini, lakini baada ya barabara hii kupatikana watu wameleta bodaboda ambazo zinatusaidia pia kuwahisha wagonjwa hospitalini,” anasema mkazi wa kisiwa cha Nafuba aliyejitambulisha kwa jina la Sophia.

Wanawake wakishiriki utengenezaji wa barabara ya kwanza katika kisiwa cha Nafuba kinachozungukwa na Ziwa Victoria katika wilaya ya Bunda, mkoani Mara hivi karibuni.
----------------------------------------
Lakini je, wazo la kujenga barabara hii lilitoka kwa nani hasa?
Kijana mzaliwa wa Nafuba, Maximillian Benjamin ndiye aliyetoa wazo la kuijenga kwa nguvu za wananchi.
“Niliona kuna mawe ya kutosha hapa kwetu Nafuba, nikawaza, nikaita wanakijiji tukakaa nikawapa wazo la kujenga barabara kwa nguvu zetu wakakubali.
“Basi mwisho wa siku tukaweka mpango, kazi ya ujenzi ikaanza baada ya mimi kuwaelekeza namna ya kuweka kamba na kupanga mawe vizuri,” anasema Benjamin ambaye amesoma taaluma ya ujenzi.
Anasema siku chache baadaye, walianza kuweka kwenye mitandao ya kijamii picha mgando na video za maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, ndipo wadau kadhaa wakajitokeza kuwaunga mkono kwa misaada ya mbalimbali.
Lakini pia, viongozi wa serikali wakiwemo kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Bunda waliweza kufika eneo la ujenzi na kusaidia ushauri wa kitaalamu.
“Hatimaye tukakamilisha hii barabara yenye urefu wa kilomita 5.6, tukajenga pia gati kwa ajili ya boti au kivuko kutia nanga kisiwani hapa katika Ziwa Victoria. Lengo la kujenga gati hili ni kuishawishi serikali itusaidie kupata kivuko,” anasema Benjamin.
Kwa mujibu kijana huyu ambaye anasema ana diploma ya ujenzi, barabara hii ilianza kujengwa Machi 2024 na kukakamilika Oktoba 2024, na kwamba ina thamani ya shilingi takriban milioni 800.
“Gharama ya ujenzi huu inakaribia shilingi milioni 800 ambazo tumeiokolea serikali. Kwa kutumia nguvu za wananchi tumemwokolea Mheshimiwa Rais Samia Sukuhu Hassan kiasi hicho cha fedha - ambacho sasa anaweza akatuletea kivuko na kutujengea kituo cha afya.
“Barabara iliyojengwa kwa mawe na moramu inadumu hadi miaka 50, cha muhimu ni kufanyiwa ukarabati wa kuwekewa molamu mara kwa mara. Kuna mtu kutoka wizarani alitembelea huku akasema hajawahi kuona wananchi wamejitolea kujenga barabara imara kama hii.
“Mbali na kuibua wazo la barabara hii, nilijitolea kusimamia ujenzi wake mwanzo - mwisho bila kulipwa hata shilingi 100. Nilisema elimu yangu isaidie jamii yangu, ili na wao wapate matunda ya kijana wao waliyemsomesha, bila kujalisha nimesomeshwa na mzazi mmoja.
“Tunajivunia barabara hii kwa sababu huduma za usafiri wa pikipiki zimefunguka hapa Nafuba, vijana wamepata ajira. Lakini pia, imerahisisha usafirishaji wa mazao na chakula kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Kwa hakika, Nafuba imefunguka sana, hata usafiri wa mitumbwi umeongezeka, kwa siku mitumbwi inafanya safari mara nne kutoka na kuingia. Kwa kifupi, barabara hii imeleta mapinduzi makubwa sana ya kimaendeleo hapa kisiwani,” anasema Benjamin.
Je, Benjamin anajisikiaje kuibua wazo la ujenzi wa barabara hii likazaa matunda?
“Cha kwanza, ninawashukuru sana wananchi wenzangu, sikuamini kwamba watanisapoti katika hili, ila ninamshukuru Mungu kwamba waliitikia wakasapoti na kazi kweli imefanyika,” anasema.
Kutokana na hatua hiyo, Diwani Namwatta anaiomba TARURA Wilaya ya Bunda kuangalia uwezekano wa kuiingiza barabara hii kwenye mtandao wake kwa ajili ya kuifanyia ukarabati mara kwa mara.
Barabara hii imesaidia kukuza biashara, kuongeza usalama na kuwezesha watu kufika kwenye huduma muhimu kama vile hospitali na shule kwa urahisi zaidi.
Mbali na usafiri, barabara hii pia imekuwa chachu ya maendeleo katika sekta za kilimo na uvuvi. Wakulima na wavuvi sasa wanapata fursa ya kusafirisha mavuno yao kwa urahisi na kuleta manufaa makubwa kwa uchumi wa familia zao.
Ujenzi wa barabara hii ni ushahidi wa uwezo wa wananchi kushirikiana kwa pamoja na kufikia maono yao ya maendeleo. Hatua hii pia, imedhihirisha jinsi ushirikiano wa wananchi na wadau wa maendeleo unavyoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii iliyozidiwa na changamoto.
Wananchi wa Nafuba wanaamini kwamba hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha kuwa kisiwa chao kinapata maendeleo endelevu na kinakuwa sehemu muhimu katika uchumi wa jimbo la Mwibara, wilaya ya Bunda na mkoa wa Mara kwa ujumla.
Hatua ya wananchi hawa kujitolea kujenga barabara yao ya kwanza inathibitisha kuwa umoja na kujitolea kuna nguvu kubwa katika kuleta mabadiliko. Kwa msaada wa wadau na juhudi za pamoja, wameweza kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya miundombinu na kupata fursa ambazo awali zilikuwa ni ndoto.
Vilevile, ujenzi wa barabara hii ni mfano wa jinsi jamii inavyoweza kuleta mabadiliko kwa kujitolea na kufanya kazi kwa pamoja, na ni ishara nzuri ya maendeleo endelevu katika eneo hili la pembezoni mwa wilaya ya Bunda.
Hivyo, kuna umuhimu kwa mamlaka za serikali wilayani Bunda na wadau mbalimbali kushirikiana na wananchi wa Nafuba kwa karibu katika utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi, ili kuhakikisha maendeleo ya kisiwa hiki.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Serengeti: Mbunge Amsabi akabidhi gari la wagonjwa Kituo cha Afya Iramba
>>Mara: Maelfu ya wanafunzi wapata 0 za kutisha Mtihani wa Taifa Kidato cha Pili 2024
>>MAKALA YA UCHAMBUZI:Dkt Machage apewe maua yake kwa moyo wa kujali afya za wananchi Tarime Vijijini
>>NECTA yatangaza matokeo ya kidato cha pili na darasa la nne 2024
No comments:
Post a Comment