
Dkt Edward Machage
Na Christopher Gamaina
Katika kuunga juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi wa Kampuni ya Win Traders Ltd, Dkt Edward Machage kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) amewiwa kuwapeleka madaktari bingwa katika Halmashauri hiyo ili kuwapatia wananchi huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu bila malipo.
Madaktari hao kutoka Taasisi ya Moyo - Dar es Salaam, Hospitali ya Rufaa Benjamin Mkapa - Dodoma na Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara, ni wale mabingwa wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kwa wazee, na magonjwa ya watoto.
Walifanya kazi kubwa ya kuhudumia wananchi zaidi ya 450 katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime - Nyamwaga Januari 4 na katika Zahanati ya Surubu katani Komaswa Januari 5, 2025.
Hatua hii ya Dkt Machage, ambayo imeleta tabasamu kwa wananchi wa Tarime Vijijini, ni uthibitisho wa jinsi anavyoguswa na afya za watu, hususan wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za vipimo na matibabu ya magonjwa makubwa.
Kwa siku mbili mfululizo, madaktari hao walitoa huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu bure kwa wazee na watoto; huduma ambazo zingepatikana kwa gharama kubwa kwenye hospitali kubwa.
Hii ni hatua muhimu inayosaidia wananchi kutoka familia maskini, ambao hawawezi kumudu gharama za matibabu makubwa. Huduma hizo hazikuishia kwenye vipimo na matibabu pekee, bali pia zilihusisha utoaji wa elimu kuhusu magonjwa hayo, ambayo mara nyingi hushughulikiwa katika hospitali kubwa maeneo ya mijini.
Katika hali ya kawaida, magonjwa ya moyo na shinikizo la damu ni miongoni mwa matatizo ya kiafya ambayo mara nyingi hayapatiwi kipaumbele katika maeneo ya vijijini kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kisasa ya afya na rasilimali. Lakini kwa upendo wa Dkt Machage, wananchi wa Tarime Vijijini wameweza kupata huduma kwa ufanisi kutoka kwa madaktari bingwa.
Wazee, ambao ni kundi la watu walio hatarini zaidi kutokana na umri wao, wameweza kunufaika na huduma hizo kutoka kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.
Watoto pia walipata huduma ya uchunguzi kuhusu magonjwa kama vile matatizo ya kupumua, kuumwa na tumbo, na matatizo mengine ya kiafya ambayo mara nyingi husababisha vifo vinavyoweza kuzuilika. Huduma hizi hapana shaka zimesaidia kuokoa maisha ya watoto wengi.
Aidha, watoto walio na magonjwa yanayohitaji matibabu ya mara moja walipata matibabu bora, jambo ambalo linaendelea kudhihirisha jinsi Dkt Machage anavyothamini afya ya kizazi kipya.
Dkt Machage, ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto na mdau wa maendeleo ya wananchi wa Tarime Vijijini, ameonesha kwa vitendo kwamba afya ya wananchi wa jamii anayotoka ni miongoni mwa vipaumbele vyake.
Hatua hii ni uthibitisho wa upendo wake wa dhati kwa jamii yake, ambapo amejitolea ili kuhakikisha inapata huduma hizo za uchunguzi, ushauri na matibabu bure, hasa wananchi wanaoishi vijijini.
Kuna wasomi na wataalamu wengi wazaliwa wa Tarime Vijijini, lakini kwa namna ya pekee, Dkt Machage ameona umuhimu wa kuwashirikisha madaktari bingwa shauku yake ya kupeleka huduma hizo muhimu kwa wananchi hao, bila kujali changamoto yoyote.
Lakini pia, hatua hii inaongeza uwazi wa jinsi wataalamu wanavyoweza kutumia nafasi zao kutatua matatizo ya kijamii kwa njia endelevu na bora. Huu ni mfano mzuri, ambapo mtaalamu anachukua hatua zinazoonekana kwa umma za kusaidia wananchi wenye changamoto za kiafya.
Dkt Machage amethibitisha kuwa siyo tu ni mzaliwa wa Tarime Vijijini na mtaalamu anayewajali wananchi wa jamii yake, bali pia ni mzalendo anayewajibika kuhakikisha kuwa watu wa vijijini na wasiojiweza kiuchumi wanasaidiwa kupata huduma za uchunguzi na matibabu bila malipo.
Wananchi wa Tarime Vijijini, hasa wazee na watoto wamefaidika sana na huduma hizo za madaktari bingwa. Wamefanyiwa vipimo, ushauri na matibabu bure kwa magonjwa ambayo wangekuwa hawana uwezo wa kupata huduma nzuri kwa gharama nafuu.
Zaidi ya hayo, hatua hii ya Dkt Machage imeongeza mwamko na elimu kuhusu afya, na imewajengea wananchi wa Tarime Vijijini imani katika huduma za afya zinazotolewa na madaktari bingwa.
Kwa ujumla, hatua ya Dkt Machage ya kuwapeleka madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kwa wazee, na magonjwa ya watoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), ni mfano wa kipekee wa jinsi alivyo na mguso chanya katika jamii yake.
Naam, hatua hii ni mfano wa kuigwa na wadau wa sekta ya afya na wapenda maendeleo katika wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara na taifa kwa ujumla ili kuleta tabasamu ya afya kwa jamii.
Basi, itoshe kusisitiza kuwa hatua hii ya Dkt Machage inadhihirisha jinsi anavyojali na kuthamini afya za wananchi kwa dhati ya moyo, na inapaswa kuigwa na watu wengine wenye nafasi ili kuhakikisha kwamba huduma bora za afya na nyingine muhimu zinawafikia wananchi wote bila kujali mazingira wanayoishi. Ubarikiwe sana Dkt Edward Machage.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>MAKALA MAALUMU:Bunda: Wananchi wajenga barabara ya kwanza kisiwani Nafuba,Dkt Mukama na wadau wengine wawapiga jeki
>>Mara: Maelfu ya wanafunzi wapata 0 za kutisha Mtihani wa Taifa Kidato cha Pili 2024
>>Waziri Mkuu wa Canada amejiuzulu
>>NECTA yatangaza matokeo ya kidato cha pili na darasa la nne 2024
No comments:
Post a Comment