NEWS

Thursday, 9 January 2025

Mara: Maelfu ya wanafunzi wapata 0 za kutisha Mtihani wa Taifa Kidato cha Pili 2024




Na Mwandishi Wetu/ Mara Online News

Maelfu ya wanafunzi wa shule za sekondari za serikali mkoani Mara wameanguka Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili wa Mwaka 2024 kwa kupata alama sifuri (0), hali ambayo imeibua maswali mengi kuhusu ubora wa elimu inayotolewa.

Matokeo ya mtihani huo yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA) Januari 4, mwaka huu, yanaonesha wasichana ndio wengi katika anguko hilo.

Baadhi ya shule za sekondari za mkoani Mara ambazo wanafunzi wengi wameshindwa mtihani huo, ni Butiama ya wilayani Butiama, ambapo wanafunzi 203 wakiwemo wasichana 109 na wavulana 94 wamepata alama 0.

Sekondari nyingine za mkoa huo na idadi ya wanafunzi waliopata alama 0 ikiwa kwenye mabano, ni Makongoro ya wilayani Bunda (164 - wasichana 83 na wavulana 81), Bulamba iliyopo Bunda DC (158 - wasichana 92 na wavulana 66), na Ingwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime- Vijijini (143 - wasichana 82 na wavulana 62),

Butuguri ya wilayani Butiama (123 - wasichana 64 na wavulana 59), Kemoramba iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma (105 - wasichana 59 na wavulana 46), na Mbogi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime- Vijijini pia (97 - wasichana 61 na wavulana 36),

Nyingine ni Nyamunga ya wilayani Rorya (94 - wasichana 48 na wavulana 46), Nyanungu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime- Vijijini (59 - wasichana 49 na wavulana 10), Bomani iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime (91 - wasichana 52 na wasichana 39), na Mugumu ya wilayani Serengeti (77 - wasichana 48 na wavulana 29).

Anguko la wanafunzi wengi katika mtihani huo limewashtua watu wengi, hasa wazazi na wadau wa elimu - wakionesha wasiwasi kuhusu mustakabali wa watoto wao na changamoto zinazowakwamisha mafanikio yao ya kitaaluma.

Walimu na wadau wametaja sababu kuu za kushuka kwa ufaulu katika sekondari za serikali mkoani Mara kuwa ni pamoja na mazingira duni ya kujifunzia, upungufu wa vifaa vya kujifunzia na baadhi ya wanafunzi kutojituma katika masomo yao.

Aidha, baadhi ya wazazi wamesema kuwa ugumu wa Maisha katika familia nyingi unachangia kushindwa kwa watoto wao kufikia viwango vya juu vya ufaulu.

Kwa ujumla, watu wengi wanajiuliza kama hatua za haraka zitachukuliwa na serikali na wadau wa maendeleo ili kuboresha elimu katika mkoa wa Mara na kukuza ufaulu wa wanafunzi kwenye mitihani ya taifa.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages