
Mwakilishi wa Nyambari Nyangwine Foundation, Sospeter Migera Paul (aliyevaa shati jeupe) akikabidhi msaada wa vitabu kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyanungu na wanafunzi leo Februari 7, 2025.
---------------------------------
Nyambari Nyangwine Foundation (NNF) imeendelea kusambaza msaada wa vitabu vya kiada na ziada kwenye shule za sekondari, ambapo leo Februari 7, 2025 sekondari tatu za kata zimekabidhiwa msaada huo.
Shule hizo ambazo kila moja imekabidhiwa vitabu vyenye thamani ya shilingi milioni mbili, ni Itiryo, Gorong’a na Nyanungu zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Makabidhiano ya vitabu katika
Shule ya Sekondari Itiryo.
------------------------------------
Akikabidhi msaada huo kwa walimu na wanafunzi wa shule hizo, Sospeter Migera Paul amesema mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Foundation amewiwa kutoa msaada huo ili kusaidia kuinua kiwango cha taaluma kwa wanafunzi na kuwawezesha kufaulu mitahani yao.
“Mheshimiwa Nyambari Nyangwine ni mdau mkubwa wa elimu, ameamua kuwekeza kwa wanafunzi, anataka watoto wetu wapate elimu ili waweze kutimiza ndoto zao za elimu,” amesema Migera ambaye ni Mwakilishi wa Nyambari Nyangwine Foundation.
Kwa upande wao walimu na wanafunzi wa shule zilizopata wameshukuru wakisema msaada huo utazisaidia kuinua taaluma.
"Tunatoa neno la asante kwa vitabu mlivyotuletea chini ya uongozi wa Nyambari Nyangwine, tunaahidi kufanya vizuri katika masomo na mitihani yetu," amesema mwanafunzi Jacklin Mororo wa Shule ya Sekondari ya Nyanungu.

Walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Gorong'a wakikabidhiwa msaada wa vitabu.
------------------------------------
Taasisi hiyo ya Nyambari Nyangwine itasambaza msaada wa vitabu vya kiada na ziada kwa shule zote zilizopo halmashauri za Tarime Vijijini na Tarime Mjini vyenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 200.
Nyambari Nyangwine ni mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2010-2015 kwa tiketi ya chama tawala - CCM.
No comments:
Post a Comment