
Mwakilishi wa Nyambari Nyangwine Foundation, Sospeter Migera Paul(wa tatu kushoto) akikabidhi msaada wa vitabu kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Muriba jana.
--------------------------------------
Nyambari Nyangwine Foundation (NNF) imeendelea kusambaza msaada wa vitabu vya kiada na ziada kwenye shule za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), ambapo jana Februari 10, 2025 sekondari tano zilikabidhiwa msaada huo.
Sekondari hizo ni Kangariani, Muriba, Bungurere, Kitawasi na Gibaso - ambazo kila moja ilipata vitabu vyenye thamani ya shilingi milioni mbili.

Makabidhiano ya msaada wa vitabu
katika Shule ya Sekondari Kangariani.
--------------------------------------
Akikabidhi msaada huo, Sospeter Migera Paul alisema Nyambari Nyangwine ambaye ni Mwenyekiti wa Nyambari Nyangwine Foundation amewiwa kutoa msaada huo kusaidia kuinua kiwango cha taaluma kwa wanafunzi ili kuwawezesha kufaulu mitahani yao na hatimaye kufikia ndoto zao za elimu.
“Mheshimiwa Nyambari Nyangwine ni mdau mkubwa wa elimu, ameamua kuwekeza kwa wanafunzi, anataka watoto wetu wapate elimu ili waweze kutimiza ndoto zao za elimu,” alisema Migera ambaye ni Mwakilishi wa Nyambari Nyangwine Foundation.

Makabidhiano ya msaada wa vitabu
katika Shule ya Sekondari Bungurere.
--------------------------------------
Walimu na wanafunzi wa shule hizo waliishukuru taasisi hiyo ya Nyambari Nyangwine na kuiomba pia kuangalia uwezekano wa kuzitatulia changamoto nyingine.
“Nitoe shukrani kwa taasisi hii kwa kutukumbuka na kutuletea vitabu vya kiada na ziada, naomba mpatapo nafasi mtukumbuke tena pia katika changamoto ya 'photocopy machine' na jengo la utawala,” alisema Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kangarian, Mwalimu Emmanuel Gwangwayi Tlatlaa.

Makabidhiano ya msaada wa vitabu
katika Shule ya Sekondari Kitawasi.
-----------------------------------
Naye Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Kangariani, Dotto Mwita Kiruka aliishukuru Nyambari Nyangwine Foundation akisema: “Mungu aendelee kumbariki Nyambari kwa msaada mliotupatia wa vitabu, tunaomba msaada wa photocopy machine na vifaa vya maabara.”

Makabidhiano ya msaada wa vitabu
katika Shule ya Sekondari Gibaso.
------------------------------------
Taasisi hiyo ya Nyambari Nyangwine inatarajia kuzifikia shule za sekondari zote zilizopo Halmashauri za Tarime Vijijini na Tarime Mjini kwa msaada wa vitabu vya ziada na kiada vyenye thamani ya shulingi milioni 200, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika uboreshaji elimu.
Nyambari Nyangwine ni mfanyabiashara, mwandishi na mchapishaji wa vitabu maarufu nchini, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime mwaka 2010-2015 kwa tiketi ya chama tawala - CCM.
No comments:
Post a Comment