
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati) akitoa maelekezo kwa wajumbe wa CDC wanaoshiriki mafunzo yaliyoandaliwa na Barrick North Mara mjini Musoma leo. Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (kushoto), Meneja Mkuu, Apolinary Lyambiko (wa pili kulia) na Menaja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi.
---------------------------------------
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amefungua mafunzo maalumu ya siku tatu Kwa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) kutoka vijiji 11 na kata tano zilizo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
Mafunzo hayo yameanza leo Februari 12, 2025 mjini Musoma na yameandaliwa na mgodi huo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), mkoani Mara.
Katika hotuba yake, Kanali Mtambi ameeleza kutoridhishwa na maendeleo ya wananchi wa vijiji vinavyopokea mabilioni ya fedha za CSR na mirabaha kutoka Mgodi wa Barrick Dhahabu wa North Mara.
Amesema vijiji hivyo vya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) vinapokea fedha hizo kila mwaka kwa ajili ya maendeleo, lakini maisha ya wananchi wake hayajaboreka kutokana na kile alichokiita viongozi kutowajibika kikamilifu katika kuzisimamia zitumike kwa ufanisi.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo.
-------------------------------------
"Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) ni miongoni mwa halmashauri zenye utajiri mkubwa hapa nchini. Mgodi unafanya kazi kubwa sana kuchangia miradi ya maendeleo kwa kutoa CSR na mrabaha, lakini bado fedha hizo hazijaleta matarajio mazuri kwa wananchi," amesema Kanali Mtambi.
Amewataka viongozi wa vijiji hivyo kuhakikisha wanaibua miradi ambayo ni kipaumbele cha wananchi na kutumia vizuri fedha hizo ili kuleta mabadiliko chanya.
Kiongozi huyo ametahadharisha kuwa hatasita kuingilia kati na kubadilisha matumizi ya fedha hizo iwapo miradi itakayoibuliwa na viongozi haitakidhi matakwa ya wananchi wa vijiji hivyo.
Ameushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kuandaa mafunzo hayo kwa viongozi hao pamoja na mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara kwa ujumla.
Amewahimiza washiriki wa mafunzo hayo kwenda kuyafanyia kazi kwa vitendo katika maeneo yao, ikiwemo kuimarisha utendaji wao wa kazi na kutatua kero za wananchi.
Kanali Mtambi ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuwataka wakazi wa eneo la Nyabirama 171 ambao bado hawajachukua fidia zao kujitokeza kuzichukua, na wale 11 waliogomea fidia ili kupisha uwekezaji wa mgodi wa North Mara waendelee kuelimishwa kuhusu umiliki wa ardhi na athari za wao kuendelea kuishi hapo wakati shughuli za mgodi zikiendelea.
Awali, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amesema wajumbe wa CDC wanaoshiriki mafunzo hayo wamo viongozi wapya waliopatikana katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita, na lengo lake ni kuwajengea uelewa juu ya utawala bora, usimamizi wa sheria, ardhi na uwajibikaji katika majukumu yao, miongoni mwa mambo mengine.

GM Lyambiko akizungumza katika mafunzo hayo.
------------------------------------
Naye Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara amesema fedha za CSR na mrabaha zinazotolewa zikitumika vizuri zitaifanya Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwa mfano bora kwa maendeleo ya jamii.
"Nawaomba viongozi wote mnaopewa mafunzo haya mkirudi katendeeni haki fedha ambazo mgodi umekuwa ukizitoa. Sijaridhika na sura ya Tarime kulingana na fedha ambazo zinatolewa, kodi wameshalipa bilioni 21, vijiji vitano vimepokea mrabaha zaidi ya bilioni sita, watu binafsi zaidi ya bilioni 65 wamelipwa.
“Mgodi naupongeza kwa kazi nzuri, lakini watendaji kafanyeni mabadiliko kusudi wananchi wapate manufaa ya hizo fedha," amesema Waitara.

Mbunge Waitara akizungumza katika mafunzo hayo.
----------------------------------
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Diwani wa Kata ya Nyarokoba, Juma Matiko wamesema yatawafanya wawajibike kwa waledi, ikiwemo kusimamia vizuri matumizi ya fedha zinazotolewa na mgodi kwa maeneo yao.
"Hii ni fursa muhimu sana kwetu viongozi kuhudhuria mafunzo haya, naupongeza mgodi kuandaa mafunzo muhimu kwetu. Naamini yatakuwa chachu ya kufanya kazi kwa umahiri na uhodari wa hali ya juu," amesema Matiko.
Washiriki wa mafunzo hayo ni pamoja na wenyeviti na watendaji wa vijiji 11, madiwani na watendaji wa kata, viongozi wa dini, wawakilishi wa makundi ya vijana, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na baadhi ya maofisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
No comments:
Post a Comment