
Mtu aliyebuni jina la nchi ya Tanzania, Mohammed Iqbal Dar mwenye asili ya India, amefariki dunia huko Birmigham, nchini Uingereza akiwa na umri wa miaka 80.
Iqbal Dar amefariki usiku wa kuamkia leo nchini Uingereza alikokua akiishi tangu mwaka 1965, baada ya kuhamia huko.
Kwa miaka zaidi ya 10, Iqbal Dar amekuwa akisumbuliwa na maradhi yaliyomfanya ashindwe kutembea.
Mohammed Iqbal Dar ni nani?
Mohamed Iqbal Dar alizaliwa Augosti 8, 1944 mkoani Tanga, alisoma katika Shule za Agha Khan na Mzumbe alikopata elimu yake ya msingi na sekondari.
Alikuwa miongoni mwa wanafunzi walioonekana wadadisi wa mambo shuleni, akishiriki mara kadhaa kwenye mashindano mbalimbali ya vipaji.
Pengine udadisi wake ulichochewa na mzazi wake, baba yake aliyekuwa daktari katika hospitali huko mikoa ya Tanga na Morogoro, alikokua anafanya kazi tangu mwaka 1930 alipokuja nchini.
Alipataje fursa ya kutunga jina la Tanzania?
Katika miaka ya 1960 mwanzoni, mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar yalikuwa katika harakati za kuunganisha mataifa hayo na kuwa taifa moja.
Katika harakati hizo, likatolewa tangazo kwenye Gazeti la Serikali la The Standard.
Sasa akiwa mwanafunzi shuleni Mzumbe, Iqbal Dar alikutana na tangazo linalomtafuta mtu ambaye atatoa wazo la jina la nchi baada ya kuunganishwa kwa Zanzibar na Tanganyika.
Kijana huyo wakati huo akiwa mdogo mwenye umri wa chini ya miaka 20, alishiriki kwa kuwasilisha jina la Tanzania, na kuibuka mshindi na kuzawadiwa shilingi 200 pamoja na medali, alizokabidhiwa na Waziri wa Habari wa wakati huo, Sheikh Idriss Abdul Wakil.
Ushindi wake ulileta furaha kwa famili na shuleni kwake, alipongezwa na kila kona.
Hatimaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa Aprili 26, 1964 ikiwa ni muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, mataifa ambayo yaliingia mkataba wa Muungano mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964 huko Zanzibar.
Jina hili la "Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar" lilibadilishwa baadaye Oktoba 28, 1964 na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria Namba 61 ya Mwaka 1964.

Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akichanganya mchanga wa Tanganyika na Zanzibar kuashiria kuungana kwa nchi hizo.
----------------------------------
Utunzi wa jina sio kitu rahisi sana. Hata majina ya watoto wetu wakati mwingine hutupa shida kutunga. Achilia mbali kutunga jina la nchi yenye watu karibu milioni 30 wakati huo.
Kutunga jina linalosubiriwa kwa hamu mpaka na marais wa nchi zote mbili. Jina la Tanzania.
Kuna wakati alipohojiwa na vyombo vya habari, alisema kwake ilikuwa moja ya kazi rahisi kufanya. Anasema alichukua herufi tatu za kutoka jina la Tanganyika (TAN), herufi tatu za jina la Zanzibar (ZAN), herufi ya kwanza ya jina lake Iqbal (I) na imani herufi ya kwanza ya dhehebu lake la kiislamu la Ahmadiyya (A).
Akaunganisha: TAN+NZAN+I+A akapata jina Tanzania, ambalo linatumika mpaka leo kama utambulisho wa taifa hilo la muungano wa nchi mbili Tanganyika na Zanzibar.
Hata hivyo, barua ya ushindi kutoka wizarani ilionesha kulikuwa na orodha ya wananchi 16, akiwemo yeye kutambulika kama washindi wa utunzi wa jina la nchi.
Iqbal Dar anajitambua kama mshindi pekee kwa kuwa ndiye aliyekabidhiwa zawadi za ushindi na kutambuliwa siku ya tukio.
Chanzo: BBC
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Mkuu wa Mkoa aagiza Mbunge wa Mwibara atafutwe kwa kukwepa vikao vya maendeleo ya wananchi
>>Chamwino: Programu ya Lipa kwa Matokeo yaondoa kero ya maji Mvumi Mission
>>Mwandishi Azam Tv ashinda Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kutoka Mara
>>TAA yasaini mkataba wa upembuzi yakinifu Uwanja wa Ndege Serengeti, serikali yatenga bilioni 1.3/-
No comments:
Post a Comment