
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Utekelezaji wa Programu ya Lipa kwa Matokeo (PforR) umefanikiwa kuondoa kero ya muda mrefu ya upatikanaji maji safi na salama kwa wananchi wa Mvumi Mission katika wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Mafanikio hayo ni kwa mujibu wa ukaguzi uliofanywa na timu ya Wizara ya Maji na Benki ya Dunia kuhusu hali ya huduma ya maji kwenye Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii Mvumi Mission wilayani Chamwino
Mratibu wa PforR katika Wizara ya Maji, Mhandisi Mashaka Sita, amesema imebainika kwamba chombo hicho cha watumia maji kimajizatiti kupiga hatua kuanzia kutoa huduma na kupanga kuongeza mtandao wa maji ili kuwafikia wananchi wengi ambapo huduma inapatikana kwa saa 12.
“Kujaza ndoo moja inatakiwa iwe chini ya dakika tano, na isizidi,” ameeleza Mhandisi Sita.
Mtaalam huyo amebainisha kuwa hicho ni kigezo cha kupima ubora wa huduma ya maji yenye kiwango katika jamii.
Diwani wa Kata ya Mvumi, Kenneth Chiute, amewashukuru wananchi wa Mvumi Mission kupatiwa huduma ya maji safi na salama na kueleza kuwa Programu ya Lipa kwa Matokeo imeondoa adha iliyokuwepo ya upatikanaji wa maji.
Chiute ametoa wito kwa watekelezaji wa programu hiyo kuifikisha kwa wananchi wa maeneo mengine ambao wanakabiliwa na uhaba wa maji.

Naye Diwani wa Viti Maalum, Shukrani Chelea, ameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa PforR kwamba sasa umeleta utulivu katika ndoa katika jamii kwa sababu huduma ya maji ilikuwa ikitafutwa usiku, na hivyo kuwafanya wanaume kutilia shaka uaminifu wa wake zao.
Katika wilaya ya Chamwino, vyanzo vingi vya maji wilayani humo ni vya chini ya ardhi, hali ambayo ni lazima mkazo uelekezwe kwenye hifadhi ya mazingira ili upatikanaji wa maji uwe endelevu.
Kazi ya ukaguzi na utekelezaji wa Programu ya Lipa kwa Matokeo imeongozwa na mtaalamu Toyoka Kudama wa Benki ya Dunia kutoka Marekani.
Tanzania ni moja ya nchi zilizofanya vizuri katika utekelezaji wa programu hiyo na kuwa darasa kwa nchi nyingine duniani.

No comments:
Post a Comment