
Na Mwandishi Wetu, Dar
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imetiliana saini na Kampuni ya Saba Engineering mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.
Akizungumza katika hafla ya kutia saini mkataba huo jijini Dar es salaam jana Februari 27, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mambokaleo alisema serikali imetenga shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja huo katika mwaka wa fedha 2024/2025.
“Kampuni ya Saba Engineering imepewa mkataba wa miezi sita na baada ya kukamilisha upembuzi yakinifu itatoa ushauri wa kitaalamu wa namna bora ya kujenga uwanja huo,” alisema Mambokaleo.
Aliongeza kuwa serikali inajenga uwanja huo ili kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA) pamoja na kurahisisha usafiri wa wananchi na mizigo kuingia mkoani Mara.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Dkt Maulid Suleiman Madeni alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na TAA kwa kuanza kutenga fedha za ujenzi wa uwanja huo akisema utaleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wananchi wa Serengeti.
“Baada ya uwanja huu kukamilika watalii watashuka moja kwa moja Serengeti na kuingia hifadhini, na wakati wa msimu wa utalii tunategemea kupata ndege hadi 100 kwa siku moja,” alisema Dkt Madeni.
Alisema uwanja huo utasaidia kuboresha uchumi wa wananchi wa halmashauri hiyo na mkoa wa Mara kwa ujumla kutokana na kujengwa kwa ofisi mbalimbali katika mji wa Serengeti kama sehemu ya uwepo wa uwanja huo.

Hafla ya utiaji saini mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti ilishuhudiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Uwanja huo, Dkt Rhimo Simeon Nyansaho.
Kujengwa kwa uwanja huoi kutasaidia kupunguza idadi ya ndege zinazotua ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kusaidia kufungua fursa za kiuchumi wilayani Serengeti na taifa kwa ujumla.
Aidha, uwanja huo utaongeza viwanja vya ndege vya mkoa wa Mara kuwa viwili baada ya serikali kutoa shilingi bilioni 35 kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege Musoma ambao pia unatarajiwa kusaidia kurahisisha usafiri kwa watalii wanaoingia katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa kutumia lango la Ndabaka lililopo wilayani Bunda.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
>>Tarime Mjini: Nyamisangura FC yatwaa ubingwa Matiko Cup 2024/2025
>>Trump na Zelensky wazozana Ikulu ya White House, mkutano wavunjika, aondoka kwa hasira
>>RC Mara aiagiza TAKUKURU kumulika michakato ya manunuzi katika miradi inayosuasua Nyanungu
>>HABARI PICHA:Mara Press Club wasaini mkataba Mradi wa Mtoto Kwanza II
No comments:
Post a Comment