NEWS

Monday, 8 December 2025

Waziri wa Mambo ya Ndani awaagiza Polisi kufuata sheria ukamataji watuhumiwa



Waziri George Simbachawene

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
-------------------

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amewataka askari wa Jeshi la Polisi kuwakamata watuhumiwa kwa kufuata misingi ya sheria na utu.

Amesema hatapenda kusikia wala kuona aina ya ukamataji unaofanywa na baadhi ya askari - wa kuvaa kininja, kutovaa sare rasmi za Polisi na kwenda kuwakamata watuhumiwa majumbani mwao usiku.

Waziri Simbachawene amesema aina hiyo ya ukamataji haikubaliki na inapaswa kukomesha mara moja.

Ametoa maelekezo hayo leo Jumatatu, Desemba 8, 2025, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Ukamataji ninaoupenda mimi ni ule wa kisheria... askari anaenda, anaripoti kwa mjumbe, mtu anajulikana yupo kazini kwake. Ya nini uende kumkamata nyumbani umevaa kininja? Tumekubaliana kuwe na ukamataji wa staha," amesisitiza.

Ameendelea kuliagiza Jeshi la Polisi kuzingatia uwiano kati ya ukubwa wa kosa na hatua zinazochukuliwa ili kuepusha matukio yanayoweza kuwatia hofu wananchi.

Amesema ukamataji ovyo wa watuhumiwa bila kufuata misingi ya sharia, na mbinu nyingine chafu umekuwa ukichoochea chuki za wananchi dhidi ya Polisi na kuathiri taswira ya jeshi hilo.

"Mambo ya kiusalama ni mengi... lazima yaendane na tukio lenyewe. Mtu kaposti kitu mtandaoni halafu anakamatwa usiku na askari wenye silaha nzito. Tumekubaliana haya hayawezi kuendelea," amesema Waziri Simbachawene.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages