NEWS

Tuesday, 25 March 2025

Uchaguzi Mkuu 2025: Dar wapendekeza Jimbo la Ukonga ligawanywe mara mbili



Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Jimbo la Uchaguzi la Ukonga mkoani Dar es Salaam sasa litagawanywa kuwa majimbo mawili ya Kivule na Ukonga iwapo mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Ushauri ya wilaya ya Ilala yatakubaliwa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Akisoma mapendekezo haya jana jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Ilala, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema jimbo mama na Ukonga sasa limependekezwa libaki na kata saba za Ukonga, Pugu, Pugu Stesheni, Gongo la Mboto, Zingiziwa, Buyuni na Chanika.

Alisema jimbo jipya la Kivule, lenye ukubwa wa kilomita za mraba 128, litakuwa na kata sita za Msongola, Majohe, Kivule, Kitunda, Kipunguni na Mzinga.

Jimbo hilo jipya, kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, litakuwa na watu 434,736 wakati jimbo la Ukonga litakuwa na watu 459,810, Chalamaila alisema.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) mwishoni mwa Februari mwaka huu ilitangaza mchakato wa kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo ilipanga zoezi hilo lifanyike kuanzia Februari 27 hadi kesho Machi 26 mwaka huu.

Tume ilisema maombi yote ya kugawa au kubadilisha jina la jimbo yawasilishwe katika kipindi kilichotajwa kwa hatua zaidi.

Chini ya Katiba ya Tanzania, Tume imepewa jukumu la kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge.

Jukumu hilo la kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi linaweza kufanywa na Tume mara kwa mara angalau kila baada ya miaka 10.

Mapendekezo ya mgawanyo wa majimbo yanatakiwa yajadiliwe katika Kamati ya Ushauri ya Wilaya kisha yawasilishwe na Katibu Tawala wa Mkoa kwenye kamati ya Ushauri ya Mkoa kwa majadiliano zaidi.

Baada ya kikao hicho cha mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa atawasilisha mapendekezo kwenye Tume vikiwemo viambatanisho.

Vigezo vinavyotumika kugawa majimbo, kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi, ni idadi ya watu ambapo majimbo ya mjini yanatakiwa yawe na wastani ya watu 600,000 wakati yale ya vijijini yawe na wastani ya watu 400,000 kwa mujibu wa Sesnsa ya 2022.

Vigezo vingine muhimu vya kugawa majimbo ni hali ya uchumi wa jimbo husika, ukubwa wake, mipaka ya kiutawala na vingi vinginevyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages