
Dkt Wilson Mukama (kushoto), akikabidhi kombe kwa washindi UMITASHUMITA Mkoa wa Mara 2025.
----------------------------------
NA MWANDISHI WETU, Tarime
MDAU wa maendeleo Dkt Wilson Mukama, amechangia Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMITA) Mkoa wa Mara 2025 shilingi milioni nne, na kuahidi msaada wa jezi kwa kila halmashauri itakayoshiriki mashindano hayo mwakani.
Dkt Mukama alitoa mchango huo alipohudhuria kama mgeni rasmi katika hafla ya kuhitimisha mashindano hayo ya mwaka huu kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Tarime wiki iliyopita.
Alifafanua kuwa shilingi milioni tatu ni kwa ajili ya maandalizi ya kambi linalofuata, na shilini milioni moja ni zawadi kwa timu zilizoshiriki mashindano hayo.
Alitoa wito kwa wadau wa michezo na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kuchangia maendeleo ya michezo, ikiwa ni pamoja na vifaa vya michezo, kujenga viwanja bora na shule za mafunzo ya michezo ili kuibua na kukuza vipaji vya michezo kwa watoto.

Aidha, Dkt Mukama alizitakia kila la heri timu zitakazoshiriki mashindano ya kitaifa ili ziweze kuuletea mkoa wa Mara ushindi kama ambavyo ilitokea miaka miwili mfululizo (2022 na 2023).
“Kwa miaka miwili mfululizo mkoa wa Mara ulishika nafasi ya kwanza kitaifa, lakini nataka kuwakumbusha kwamba nafasi ya tatu ambayo mkoa wa Mara ulishika mwaka jana siyo nafasi yenu, hivyo rudini kwenye nafasi yenu ya kwanza.
“Tunatarajia kuanzia mwaka huu na kuendelea mkoa wa Mara utaonesha mafanikio makubwa katika michezo kwani utarudi kwenye nafasi yake,” alisema Dkt Mukama na kushangiliwa na umati mkubwa wa washiriki.

“Viongozi bora ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa letu, hivyo kila mmoja wetu anao wajibu wa kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu,” alisisitiza.
Mashindano ya UMITASHUMITA Mkoa wa Mara 2025 yalizinduliwa Aprili 9 na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi.
Kaulimbiu ya mashindano hayo mwaka huu inasema “Viongozi Bora ni Msingi wa Maendeleo ya Taifa letu, Shiriki Uchaguzi Mkuu kwa Amani na Utulivu”.
No comments:
Post a Comment