
Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Nyansaho Foundation, Dkt Rhimo Nyansaho (kushoto), akimkabidhi nyumba hizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota, wiki iliyopita.
--------------------------------------
NA MWANDISHI WETU, Serengeti
NYANSAHO Foundation (NF) imejitolea kugharimia ujenzi wa nyumba tatu za walimu katika Shule ya Sekondari Musati iliyopo kata ya Kebanchabancha, wilaya ya Serengeti, mkoani Mara.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na taasisi hiyo kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya utoaji utoaji wa elimu.
“Tulipofika Shule ya Musati kujadili taaluma tulibaini mapungufu kadhaa, ikiwemo ukosefu wa nyumba za walimu, ndipo Nyansaho Foundation ilichukua hatua ya ujenzi wa nyumba hizi ili kuboresha mazingira ya kufundisha.
“Kama mwalimu hana mahali pa kuishi hawezi kufundisha vizuri wala kuwasaidia watoto wetu kujifunza Kwa usahihi. Nyumba hizi za kisasa zimeunganishwa na mfumo wa maji na umeme, nitoe rai mzitunze vizuri,” Mwenyekiti na Mwanzilishi wa NF, Dkt Rhimo Nyansaho alisema katika hafla ya kukabidhi nyumba hizo wiki iliyopita.
Kuhusu changamoto ya bweni, Dkt Nyansaho alisema wameshawasiliana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) likaahidi kujenga kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka mbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kemirembe Lwota, aliipongeza Nyansaho Foundation kwa jitihada kubwa kuchangia uboreshaji wa mazingira ya elimu katika shule mbalimbali.
“Elimu ndiyo ufunguo wa maisha yetu kila pembe ya wilaya ya Serengeti, Nyansaho Foundation imeendelea kuboresha miundombinu ya kujinfunza na kufundishia, mfano ni hizi nyumba tulizopokea leo,” alisema Kemirembe.
Naye Afisa Elimu Kata ya Kebanchabancha, Mwalimu Adam Nyakimori, alisema “Nyumba hizi tatu kila moja ni Kwa ajili ya familia mbili, tunatarajia zitakuwa chachu ya kuimarisha taaluma katika shule hiyo.”
No comments:
Post a Comment