NEWS

Tuesday, 15 April 2025

Mgodi wa Barrick North Mara watenga bilioni 4.687/- nyingine za miradi ya kijamii Tarime Vijijini



Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu 
wa North Mara, Apolinary Lyambiko.
---------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu

Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) imeendelea kunufaika na uwepo wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara baada ya mgodi huo kutenga kiasi kingine cha shilingi zaidi ya bilioni 4.687 kutokana na uzalishaji wa mwaka 2024 kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii.

Hatua hiyo imekuja miezi michache baada ya mgodi huo kutoa shilingi zaidi ya bilioni tisa kutokana na uzalishaji wa mwaka 2023 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii mwaka huu katika halmashauri hiyo.

Fedha hizo zinatolewa kupitia mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) wa kampuni ya Barrick inayoendesha mgodi wa North Mara kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals tangu mwaka 2019.

“Kutokana na uzalishaji wa mwaka 2024, mgodi umetenga shilingi 4,687,961,715 kwa ajili ya miradi ya jamii, ikiwemo kupanua mradi wa maji wa Matongo ufikie vijiji vingine - tukianza na kijiji cha Kewanja,” Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko, aliwambia waandishi wa habari mgodini hapo Ijumaa iliyopita.

Alisema mchakato wa kuibua miradi mipya na upanuzi wa mradi huo wa maji unaendelea.

GM Lyambiko alibainisha kwamba kwa sasa mgodi huo unaendelea kutekeleza miradi 101 ya CSR kwenye kata 26 zenye vijiji 88 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

“Miradi ya CSR ambayo imepitishwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inaendelea kutekelezwa kwa gharama ya shilingi 9,049,264,380.

“Miradi hiyo inagusa nyanja zote muhimu za maendeleo, ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara, uwezeshaji kiuchumi na mazingira,” alisema GM Lyambiko.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo alisema mgodi huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kukabiliana na wavamizi wa mgodi wanaokwenda kuiba mawe yenye dhahabu.

“Mfano msimu huu wa mvua na tunapokaribia msimu wa uchaguzi mara nyingi kunakuwa na ongezeko la wavamizi,” alisema Meneja Mkuu huyo na kuwaomba waandishi wa habari kutumia kalamu zao kukemea vitendo hivyo vya kihalifu sambamba na kuhamasisha mahusiano kati ya mgodi huo na jamii.

“Vitendo vya uvamizi siyo sahihi, tuvikemee," alisisitiza GM Lyambiko huku akitaja faida lukuki zinazotokana na uwepo wa uwekezaji wa mgodi huo, ikiwemo fursa za ajira na biashara kwa wakandarasi wakiwemo wazawa.

Aidha, alisema mgodi wa North Mara unakabiliwa na kikwazo cha watu ambao hawajachukua fidia za maeneo na mali zao ili kupisha upanuzi wa shughuli za uchimbaji katika shimo la wazi la Nyabigena.

“Mpaka sasa asilimia 81 ya wananchi hao wameshafidiwa, na bado kuna watu 135 waliofanyiwa tathmini ya mali zao lakini hawajaja kutia saini ya mkataba wa fidia. Kadhalika, wapo wengine 11 ambao waligomea kabisa shughuli ya uthamini,” alisema GM Lyambiko.

Kutokana na hali hiyo, waandishi wa habari wana jukumu la kutumia taaluma yao kuelimisha jamii kuhusu mchango mkubwa wa maendeleo unaotolewa na mgodi huo kwa wananchi wa Tarime na taifa kwa ujumla.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages